HATIMAYE WAZIRI MWAMBE AUONA MWEZI POLISI KISUTU YAMPATIA DHAMANA

 Na Arushadigital – Dar es Salaam

ALIYEKUWA Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Geofrey Mwambe, ameachiwa kwa masharti ya dhamana katika Kituo cha Polisi cha Kati (Central Police), baada ya kushikiliwa kwa muda huku uchunguzi ukiendelea.


Hatua hiyo imeifanya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuyaondoa rasmi maombi Na. 289778/2025, yaliyokuwa yamewasilishwa na Mwambe kupitia wakili wake, Hekima Mwasipu, akiomba dhamana.


Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama jana, Wakili Mwasipu amesema waliwasilisha ombi la kuyaondoa maombi hayo baada ya kubainika kuwa mteja wake tayari alikuwa ameachiwa kwa dhamana katika kituo cha polisi.


“Baada ya mteja wetu kuachiwa kwa dhamana tangu Alhamisi, Desemba 14, 2025, hakukuwa na msingi wa kisheria wa kuendelea na maombi yaliyokuwa mbele ya mahakama,” amesema Mwasipu.


Ameeleza kuwa hoja hiyo haikupingwa na upande wa Jamhuri, hali iliyoiwezesha mahakama kuridhia na kuyaondoa rasmi maombi hayo.


Hata hivyo, hatua ya kumshikilia mtuhumiwa kwa muda mrefu kabla ya kuachiwa kwa dhamana imeibua mjadala mpana kuhusu haki za mtuhumiwa na wajibu wa vyombo vya dola, hususan suala la kuwafikisha watuhumiwa mahakamani kwa wakati kama inavyotakiwa kisheria.


Kwa mujibu wa wataalamu wa sheria, ingawa polisi wana mamlaka ya kufanya uchunguzi, sheria inaweka mipaka ya muda wa kumshikilia mtuhumiwa bila hatua za mahakama, ili kulinda misingi ya haki na utawala wa sheria.


Kwa sasa, inatarajiwa kuwa taratibu nyingine za kisheria zitaendelea kulingana na matokeo ya uchunguzi unaoendelea, huku jamii ikiendelea kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo kwa karibu.

Post a Comment

0 Comments