WAZAZI WA JAMII YA WAFUGAJI NGORONGORO WALIA KUPOKONYWA WATOTO WAO NA MFANYABIASHARA KWA MIAKA 10 AKIWABADILISHA MAJINA ,WAMWOMBA WAZIRI GWAJIMA KUINGILIA KATI

Na Joseph Ngilisho, NGORONGORO

 

SIMANZI, machozi na Vilio vimetawala katika familia tatu za jamii ya wafugaji  kitongoji cha Olobo, kijiji cha Lopulu, wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, kufuatia wazazi wanaodai kutowaona watoto wao waliochukuliwa miaka 10 iliyopita wakidaiwa ni yatima kwa ahadi ya kusomeshwa lakini hawajawahi kurejea nyumbani hadi leo.

 

Wazazi wa watoto hao wanamuomba Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dkt. Dorothy Gwajima, kuingilia kati ili kusaidia kufanikisha upatikanaji wa watoto wao, ambao kwa mujibu wao hawajawahi kutoa taarifa yoyote tangu mwaka 2015.


Wazazi hao watatu — Naramat Ngai, Narang'a Koila na Ndiako Salangat — walizungumza kwa uchungu mkubwa nyumbani kwao, wakidai kuwa licha ya juhudi za kutafuta taarifa, hawajawahi kufanikiwa kuwaona wala kujua hali zao.“Hatujui kama wako hai au wamekufa”



Wakizungumza kwa hisia kali leo desemba 11,2025, walisema wameishi miaka 10 ya mateso, maswali yasiyo na majibu na kutokuwa na uhakika kama watoto wao bado wako hai. Waliwataja baadhi ya viongozi wa eneo hilo pamoja na Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Ngorongoro, Benezet Bwigizo, kuwa walihusika katika mchakato wa kuwaruhusu watoto kuchukuliwa na mfadhili aliyedai kutaka kuwasomesha.

Naramat Ngai alisema mtoto wake, Kitindi Ngai, alichukuliwa mwaka 2015 akiwa na umri wa miaka minne.

> “Miaka yote hii sijawahi hata kusikia sauti yake. Naomba serikali inisaidie nipate mtoto wangu akiwa hai,” alisema kwa majonzi.


Naye Narang’a Koila alisimulia jinsi mtoto wake Seyo Kwela, ambaye alikuwa akiishi kwa ndugu yake, alivyodaiwa kuchukuliwa kwa madai ya kutafutiwa elimu na udhamini.

Anadai kusikia kuwa sasa anaishi Arusha kwa mfanyabiashara Ghulam Hussein, na kwamba jina lake limebadilishwa kuwa la Kiislamu, jambo ambalo limezua maswali zaidi kwa familia hiyo ambayo haina utamaduni wa kubadili majina ya watoto.

Ndiako Salangat alisema mtoto wake Nginyi Salangat, aliyekuwa na miaka mitano wakati akichukuliwa, angekuwa na miaka 17 kwa sasa."Naona kama mtoto wangu ameuzwa”

> “Nimehangaika hapo halmashauri kwa ofisa ustawi wa jamii mara nyingi bila msaada. Kwa hali ilivyo, naanza kuamini huenda mtoto wangu ameuzwa,” alisema akiwa na uchungu mwingi.

Wazazi hao walisema wamefikia hatua ya kuuza mifugo yao, wakitafuta fedha za kusafiri kutafuta watoto katika maeneo mbalimbali bila mafanikio.

 

Akizungumzia tuhuma hizo, Benezet Bwigizo alikiri kuwepo kwa tukio hilo, akisema lilifanyika mwaka 2015 baada ya mfanyabiashara Ghulam Hussein kufika kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daud Ntibenda, kuomba kusaidia watoto wanne kutoka jamii ya kifugaji ikiwa ni sehemu ya kutoa sadaka kwa namna hiyo.

Kwa mujibu wa Bwigizo,Mkuu wa Mkoa Ntibenda alimuelekeza Mkuu wa Wilaya wa wakati huo, Hashimu Mgandilwa ambaye naye alimwelekeza afsa ustawi wa jamii Benezet Bwigizo ambaye naye alielekeza kwa viongozi wa kitongoji kufuta watoto waliotajwa kuwa na uhitaji.

Baada ya kupatikana walifanya utaratibu wa kuwasafirisha kwenda kwa mfadhili u chini ya uangalizi wa afisa huyo wa ustawi wa jamii

> “Watoto hao bado wanasoma chini ya ufadhili wa Ghulam Hussein. Tumeagiza waletwe nyumbani wikiendi hii wakutane na wazazi wao,” alisema Bwigizo.


Hata hivyo, wazazi walisema miaka 10 ni muda mrefu mno kwa mtoto kutosalimia, kutopiga simu wala kurudi nyumbani.

Mfanyabiashara Ghulam Hussein, alipotafutwa, alikataa kulizungumzia suala hilo na kuelekeza maswali yote kwa Afisa Ustawi wa Jamii au Katibu Tawala wa Wilaya.


MEMUTE: “Watoto warejeshwe, lakini kwanini siri kwa miaka 10?”

Mkurugenzi wa Memute Organization, Rose Njilo, alipoulizwa kuhusu hatua ya kuwarejesha watoto hao kwa wazazi wao, aliunga mkono uamuzi huo lakini akalaani vikali mazingira ya usiri yaliyolitawala suala hilo kwa miaka yote.

> “Ni jambo jema kama watoto hao wataletwa nyumbani, lakini tunalaani namna ambavyo suala hili limefanyika kwa kificho na kuwaacha wazazi bila amani kwa muda wote huu,” alisema Njilo.


Aliongeza kuwa, kutokana na muda mrefu walioishi mbali na familia zao, watoto hao sasa huenda hawajui kabisa lugha ya kwao ya Kimasai, huku wazazi wao nao wakikosa uelewa wa Kiswahili, hali ambayo itafanya mawasiliano kuwa changamoto kubwa.

> “Tuna raha ya kurudi kwao, lakini pia tuna wasiwasi: watoto hawa watawasiliana vipi na wazazi wao? Hii imezua pengo la kijamii, kiutamaduni na kihisia ambalo halikupaswa kutokea,” alisema.

Njilo alisema shirika lake litaendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha suala hilo linafanyiwa uchunguzi wa kina, na kwamba miiko ya ulinzi wa mtoto na ridhaa ya mzazi lazima izingatiwe kwa wakati wote.

Wazazi hao waliishukuru MEMUTE ORGANIZATION kwa kuwasimamia na kuwasaidia sauti yao ifike serikalini, wakisema bila msaada huo wangekuwa bado kimya huku wakiendelea kuteseka moyoni.







--ends..

Post a Comment

0 Comments