KIJAJI ATOA MWELEKEO MZITO NGORONGORO
Aapisha Kamishna Mkuu, Azindua Bodi Mpya ya NCAA
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, ametoa mwelekeo mzito wa kisera na kiutendaji kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), akisisitiza kuwa mustakabali wa hifadhi hiyo ya kimataifa lazima uendeshwe kwa mizani madhubuti ya uhifadhi endelevu, biashara yenye tija na manufaa ya moja kwa moja kwa jamii.
Akizungumza leo Januari 29,2026 jijini Arusha katika hafla ya kumuapisha Kamishna Mkuu wa NCAA, Abdul-Razaq Badru, sambamba na uzinduzi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi, Waziri Kijaji alisema Ngorongoro inaingia katika kipindi nyeti kinachohitaji uongozi thabiti, maamuzi magumu na uwajibikaji wa hali ya juu ili kulinda hadhi yake kama urithi wa Taifa na Dunia.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa Serikali, wadau wa uhifadhi, menejimenti na watumishi wa NCAA pamoja na viongozi wa jamii zinazozunguka eneo la Ngorongoro.
Waziri Kijaji alisema uteuzi wa Kamishna Mkuu huyo uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, unaakisi imani kubwa ya Serikali kwa uwezo wake wa kuiongoza NCAA katika kutimiza malengo ya Taifa, ikiwemo dira ya kufikisha idadi ya watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030.
Maelekezo Sita Mazito
Katika hotuba yake, Waziri Kijaji alitoa maelekezo sita mahsusi kwa Kamishna Mkuu mpya, akimtaka,
Kulinda ikolojia ya Ngorongoro ili iendelee kuvutia, kwa kuhakikisha misitu, wanyamapori na viumbe hai vinahifadhiwa ipasavyo.
Kuboresha huduma za malazi, kwa kuongeza idadi ya vitanda kutoka 1,555 hadi kufikia 2,590 ili kukidhi mahitaji ya utalii wa hadhi ya juu,Kushirikisha wataalamu kubuni mazao mapya ya utalii kila mwaka, kwa lengo la kuongeza angalau kivutio kimoja kipya kila mwaka.
Kuboresha ubora wa huduma za utalii ili kuongeza ushindani wa Ngorongoro katika soko la kimataifa,Kuimarisha mahusiano kati ya NCAA, wadau wa utalii na mamlaka nyingine za Serikali.
Kutekeleza majukumu kwa kuongozwa na kauli mbiu ya “Kazi na Utu”, kwa kuzingatia ustawi wa jamii na watumishi wa Mamlaka.
“Kuvishwa cheo hiki si heshima tu, bali ni mzigo mkubwa wa wajibu. Serikali inatarajia kuona matokeo ya moja kwa moja katika uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii,” alisisitiza Waziri Kijaji.
Akizungumzia utendaji wa Kamishna Badru katika kipindi cha miezi saba tangu ateuliwe, Waziri Kijaji alisema Serikali imeridhishwa na mwelekeo aliouweka, hususan katika kuimarisha uhifadhi, kusimamia maslahi ya watumishi na kuongeza mapato ya Mamlaka.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, makadirio ya mapato ya NCAA yameongezeka kwa kiwango kikubwa, kutoka takribani Sh bilioni 250 hadi zaidi ya Sh bilioni 550 kwa mwaka wa fedha 2025/2026, hatua aliyoitaja kuwa ushahidi wa uongozi makini na usimamizi unaozingatia tija.
Alikumbusha kuwa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yako wazi: Ngorongoro lazima iendeshwe kwa misingi miwili mikuu—uhifadhi na biashara—bila kuathiri ikolojia yake ya kipekee.
Bodi Mpya, Majukumu Mapya
Akizindua Bodi mpya ya Wakurugenzi ya NCAA, Waziri Kijaji alisema bodi hiyo ina wajibu wa kimkakati katika kusimamia sera, kuishauri Menejimenti na kuhakikisha Mamlaka inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Serikali.
Aliitaka bodi hiyo kushirikiana kwa karibu na Menejimenti katika kubuni mazao mapya ya utalii, kuvutia uwekezaji, kuboresha miundombinu ikiwemo huduma za malazi, pamoja na kuimarisha matangazo ya vivutio vya Ngorongoro katika soko la kimataifa.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mahusiano kati ya hifadhi na jamii zinazozunguka eneo hilo, akibainisha kuwa mafanikio ya uhifadhi hayawezi kupatikana bila wananchi kunufaika moja kwa moja.
“Jamii ni wadau wakuu wa uhifadhi. Lazima waone faida ya moja kwa moja ili kulinda urithi huu wa taifa kwa kizazi cha sasa na kijacho,” alisema.
Badru Aahidi Uongozi Thabiti
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa NCAA, Abdul-Razaq Badru, alisema cheo alichopewa ni dhamana kubwa ya kitaifa, akiahidi kuiongoza Ngorongoro kwa misingi ya nidhamu, uwajibikaji na ufanisi wa hali ya juu.
“Cheo hiki si heshima binafsi, bali ni dhamana ya kulinda urithi wa taifa na hadhi ya Tanzania mbele ya dunia,” alisema Badru.
Alisema lengo la uongozi wake ni kuifanya Ngorongoro kuwa kituo cha utalii wa hadhi ya juu (premium safari destination) kinachochangia kikamilifu katika uchumi wa Taifa bila kuhatarisha ikolojia yake.
Hafla hiyo imetajwa kuwa mwanzo wa sura mpya ya uongozi ndani ya NCAA, huku Serikali ikionesha dhamira thabiti ya kuilinda, kuikuza na kuisimamia Ngorongoro kama urithi wa Taifa na Dunia.
Mwisho.
















0 Comments