KUHAMISHWA KWA OCD MATAGI KWAPONGEZWA, MALALAMIKO YA UBABE ,CHUKI BINAFSI YAFICHUKA
By Arushadigital | ARUSHA
ARUSHA. Uhamisho wa aliyekuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha (OCD), Georgina Matagi, umeibua hisia tofauti jijini hapa, huku baadhi ya wananchi, viongozi, askari polisi na waandishi wa habari wakieleza kuwa hatua hiyo imewapa faraja kutokana na madai ya mwenendo wa uongozi walioueleza kuwa ulikuwa na ukali uliopitiliza, kutosikiliza malalamiko na matumizi ya mahabusu kama njia ya kushughulikia baadhi ya watu waliokinzana na uamuzi wake.
Baadhi ya watu waliozungumza na mwandishi wa habari hii kwa sharti la kutotajwa majina, walidai kuwa katika kipindi cha uongozi wake, viongozi wakiwemo madiwani pamoja na waandishi wa habari waliwahi kuwekwa mahabusu, huku baadhi yao wakidai kuwa walipojaribu kufuatilia kuachiwa kwao walielezwa kuwa hawangeachiliwa hadi pale OCD mwenyewe atakapoamua.
Kwa mujibu wa madai hayo, baadhi ya wasaidizi wake walisisitiza kuwa mhusika “hatoki mpaka OCD aamue vinginevyo,” kauli ambayo ilizua maswali miongoni mwa baadhi ya watu kuhusu mamlaka yaliyokuwa yakitumika katika maamuzi hayo.
Mmoja wa watu waliodai kushuhudia matukio hayo alisema baadhi ya viongozi walipokuwa wakifuatilia suala la dhamana waliambiwa kuwa uamuzi wa mwisho ulikuwa mikononi mwa OCD.
“Kulikuwa na kauli kwamba mtu hatoki mpaka OCD aamue vinginevyo. Watu wengi walijiuliza nguvu hiyo ilitoka wapi, kwa sababu dhamana na taratibu za kisheria zina utaratibu wake,” alisema.
WANAHABARI WALAZIMIKA KUMTAFUTA IGP
Madai hayo yanaelezwa pia kuwahi kuwalazimisha baadhi ya wanahabari kutumia njia za juu za uongozi wa Jeshi la Polisi kutafuta msaada pale walipoona wenzao wamekamatwa au kuzuiliwa kwa muda waliouona kuwa haukuwa wa kawaida.
Baadhi ya wanahabari wamedai kuwa walifika hatua ya kupiga simu kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) kuomba msaada katika kuhakikisha wenzao wanapata dhamana au wanaachiliwa kwa mujibu wa taratibu.
Kwa mujibu wa madai yao, katika baadhi ya matukio hatua hiyo ilisaidia kuwezesha waandishi waliokuwa wamezuiliwa kupata dhamana au kuachiliwa bila masharti, jambo lililoongeza hisia kwamba kulikuwa na mvutano kati ya baadhi ya wanahabari na uongozi wa Polisi Wilaya ya Arusha.
Mwandishi mmoja alisema hali hiyo ilikuwa ikiwatia hofu baadhi ya wanahabari, hasa pale walipokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kuripoti matukio yanayohusu Jeshi la Polisi.
“Tulilazimika wakati mwingine kutafuta msaada kutoka juu kwa sababu tuliona mwenzetu amezuiliwa na hakuna maelezo yanayotupa uhakika wa lini ataachiwa. Ilibidi viongozi wa juu wa Jeshi waingilie kati,” alidai.
MADIWANI NA VIONGOZI WAKUMBUSHWA
Mbali na wanahabari, baadhi ya wananchi na viongozi wa kisiasa wameeleza kuwa waliguswa na namna baadhi ya viongozi, wakiwemo madiwani, walivyowahi kukabiliwa na hatua za kukamatwa na kuwekwa mahabusu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi yao walidai kuwa hatua hizo ziliwafanya viongozi hao kukaa mahabusu kwa muda mrefu na kusababisha malalamiko kutoka kwa wananchi waliokuwa wakiwafuatilia.
Kwa baadhi ya wakazi wa Arusha, kuhamishwa kwa Matagi sasa kunatazamwa kama fursa ya kujenga upya mahusiano kati ya Jeshi la Polisi, viongozi wa jamii, wanahabari na wananchi.
ASKARI WENYEWE WALALAMIKA
Malalamiko hayakuishia kwa wananchi na wanahabari pekee. Baadhi ya askari polisi, ambao waliomba majina yao yahifadhiwe, walidai kuwa walikuwa wakikabiliwa na mazingira magumu ya kiutendaji, wakimtuhumu Matagi kutumia hatua za kinidhamu kwa mtindo waliouona kuwa wa kuogopesha.
Baadhi yao walidai kuwa askari waliweza kupelekwa “lokapu” kwa maamuzi ambayo waliona hayakuwa yakitanguliwa na kusikilizwa kwa kina.
Mmoja wa askari hao alisema kuhamishwa kwa Matagi kumepokelewa kwa furaha na baadhi ya askari, akidai kuwa wenzake waliona kama wamepata nafasi ya kuanza ukurasa mpya wa uongozi.
“Wapo ambao walifurahi sana baada ya kusikia amehamishwa. Baadhi yao waliona kama mzigo umeondoka. Lakini sisi hatutaki kutajwa kwa sababu bado tupo kazini,” alisema.
MAMBO YAIBUA MJADALA WA UWAJIBIKAJI
Madai haya, iwapo yatathibitishwa rasmi, yanaibua mjadala kuhusu mipaka ya mamlaka ya makamanda wa polisi katika ngazi za wilaya, namna ya matumizi ya mamlaka ya kuwakamata na kuwashikilia watu pamoja na umuhimu wa kuzingatia sheria, haki za msingi na taratibu za dhamana.
Hata hivyo, madai ya wananchi, askari na wanahabari hayajathibitishwa kwa upande wa Jeshi la Polisi, na juhudi za kupata ufafanuzi rasmi kuhusu tuhuma hizo pamoja na sababu za uhamisho wa Matagi zinaendelea.
Kwa sasa, jambo moja linaloonekana wazi ni kwamba kuondoka kwa Matagi katika nafasi hiyo kumeacha mjadala mzito Arusha, huku baadhi ya wananchi wakitumaini kuwa uongozi mpya utajenga mazingira ya ushirikiano, uwajibikaji na kuheshimu taratibu za sheria kati ya Polisi na jamii.

Post a Comment