MWEKEZAJI RAIA WA KIGENI AILILIA SERIKALI KUFUATIA KUFUNGIWA BARABARA YA UMMA ARUSHA
Gesso Bajuta atajwa kuifunga kinyume cha sheria; Serikali ya Mtaa yathibitisha ni barabara ya umma
Na Arushadigital -ARUSHA
MWEKEZAJI raia wa kigeni, Ugur Karas, ameomba Serikali iingilie kati mgogoro ulioibuka katika Mtaa wa Ngaramtoni ya Chini, Kata ya Olmot, Jiji la Arusha, baada ya kudai kufungiwa barabara ya umma inayoelekea katika makazi na eneo lake la uwekezaji—hatua anayoeleza kuwa ni kinyume cha sheria na inayotishia mazingira ya uwekezaji nchini.
Karas, ambaye ni mwanzilishi na mwekezaji wa Tupo Pamoja Foundation, alisema kufungwa kwa barabara hiyo kumeathiri moja kwa moja shughuli zake za kijamii na kiuchumi, zikiwemo uendeshaji wa makazi, bungalows, pamoja na miradi ya kijamii inayowanufaisha wakazi wa maeneo ya Kuchimba na Kisima.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Karas alisema barabara hiyo imekuwepo kwa muda mrefu na imekuwa ikitumika kama njia halali ya umma, lakini ilifungwa ghafla bila taarifa wala maelezo ya kisheria, wakati yeye akiwa nje ya nchi.
“Nilirejea Arusha nikakuta njia yangu ya kuingia nyumbani na kwenye uwekezaji wangu imefungwa. Nilipohoji nikaambiwa ni makosa na itafunguliwa, lakini hadi sasa haijafunguliwa,” alisema Karas kwa masikitiko.
GESSO BAJUTA ATAJWA KUFUNGA BARABARA
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa barabara hiyo inadaiwa kufungwa na mfanyabiashara Gesso Bajuta, hali iliyozua malalamiko makubwa si tu kutoka kwa mwekezaji huyo wa kigeni bali pia kwa wakazi wengine wanaoitumia barabara hiyo kwa shughuli zao za kila siku.
Karas alisema kufungwa kwa barabara hiyo kumesababisha wafanyakazi wake kushindwa kufika kazini kwa wakati, magari kushindwa kuingia katika eneo la uwekezaji, na wakati mwingine kulazimika kulala nje ya eneo hilo—hali inayosababisha hasara kubwa, usumbufu wa kiusalama na kuathiri maisha ya watu wengi.
“Hili si tatizo langu peke yangu. Ni barabara ya umma inayotumiwa na wananchi wengi. Kitendo cha mtu mmoja kuifunga bila kufuata sheria kinatuma ujumbe mbaya kwa wawekezaji,” alisema.
Aliongeza kuwa hoja zinazotolewa za kiusalama au za mifugo haziwezi kuwa msingi wa kisheria wa kufunga barabara ya umma, akisisitiza kuwa tangu aishi katika eneo hilo hajawahi kushuhudia vitendo vya uhalifu vinavyohalalisha hatua hiyo.
SERIKALI YA MTAA YATHIBITISHA: NI BARABARA YA UMMA
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ngaramtoni ya Chini, Ibrahim Urasa, alithibitisha kuwa barabara hiyo ni mali ya umma na hakuna mtu binafsi mwenye mamlaka ya kuifunga bila kibali halali cha kisheria kutoka mamlaka husika.
Urasa alisema ofisi yake ilipokea taarifa za kufungwa kwa barabara hiyo kwa njia ya simu na mara moja ilianza kufuatilia suala hilo kwa kuwaita wahusika wote wakiwemo waliotajwa kuifunga barabara hiyo.
“Hii ni barabara ya wananchi. Tumemwita mfanyabiashara anayetajwa kuifunga, Gesso Bajuta, afike ofisini atoe maelezo na alete nyaraka za kuthibitisha kama ana mamlaka ya kufanya hivyo,” alisema Urasa.
Aliongeza kuwa barabara hiyo ni kiungo muhimu kati ya Ngaramtoni Juu, Kisongo na Olmot, na hutumiwa na wakazi, wafanyabiashara pamoja na vijana zaidi ya 30 wanaopata ajira katika eneo hilo. Aidha, Serikali ya Mtaa imeahidi kufuatilia kwa umakini hatua ya Bajuta ili kujua amepata wapi jeuri ya kufunga barabara hiyo, huku ikisisitiza sheria iheshimiwe.
Karas alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa sera zake za kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, lakini akasisitiza umuhimu wa sera hizo kusimamiwa kikamilifu hadi ngazi za chini ili kulinda haki za wawekezaji na wananchi.
“Naipenda Tanzania na wananchi wake. Tunaishi kwa amani na tunasaidia jamii. Ninachoomba ni haki, sheria iheshimiwe na Serikali ilinde wawekezaji pamoja na wananchi wake,” alisema.
Kwa upande wake, Gesso Bajuta, akizungumza kwa kifupi kwa njia ya simu, alisema aliamua kufunga barabara hiyo kutokana na hofu ya mifugo kupita karibu na eneo lake, akidai hatua hiyo ilikuwa ya kujilinda dhidi ya uwezekano wa maambukizi ya magonjwa.
Ends..










0 Comments