RC Makala Aagiza Msaada wa Kisheria Kusogezwa Hadi Vijijini
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
MKUU wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makala, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinawafikia wananchi wote, hususan wale wanaoishi katika maeneo ya pembezoni na wasiokuwa na uwezo wa kugharamia gharama za kisheria.
Kauli hiyo imetolewa leo januari 28,2026 wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya kitaifa kwa mawakili wa Serikali kuhusu msaada wa kisheria, yaliyofanyika jijini Arusha. CPA Makala ambaye alimwakilisha waziri wa katiba na Sheria ,Juma Homera alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha upatikanaji wa haki, usawa na utawala wa sheria nchini.
“Migogoro mingi ya kijamii inatokana na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu haki na wajibu wao wa kisheria. Ni jukumu letu kuhakikisha elimu ya sheria inafika hadi kwa kila mwananchi,” alisema CPA Makala.
Aliongeza kuwa utoaji wa msaada wa kisheria unasimamiwa kwa mujibu wa Sheria ya Msaada wa Kisheria, Sura ya 21, iliyoundwa kusaidia wananchi wasio na uwezo wa kifedha. Pia aliwataka mawakili kushirikiana na jamii kupambana na mila na desturi zinazosababisha ukosefu wa haki kwa baadhi ya makundi.
Mafunzo hayo, alisema, yataongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za kisheria na kuchangia katika kujenga taifa lenye amani, usawa na haki kwa wote.
Awali wakili Richard Odongo ambaye ni Mkurugenzi wa wa sheria ofisi A waziri Mkuu TAMISEMI alisema aerikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeanza utekelezaji wa mkakati wa kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinashuka hadi ngazi ya chini kabisa, kutokana na kuongezeka kwa migogoro ya ardhi, ndoa na mirathi inayolikumba jamii mbalimbali nchini.
“Mawakili wengi wa kujitegemea wanapatikana mijini, lakini changamoto za kisheria zipo zaidi vijijini. Serikali imeamua kupeleka wanasheria wa umma moja kwa moja kwa wananchi,” alisema Wakili Odongo.
Alisema huduma hizo zitatolewa bila malipo (pro bono) na wanasheria wa umma wanaolipwa mishahara na serikali, kwa lengo la kupunguza migogoro, kulinda haki za wananchi na kupunguza mzigo wa kesi mahakamani.
Aidha, Wakili Odongo alifafanua kuwa mafunzo haya ni hatua ya mwanzo, na yanatarajiwa kufuatiwa na ushirikishaji wa wanasheria wa mamlaka 186 za Serikali za Mitaa, ili kuhakikisha msaada wa kisheria unashuka hadi kila kata, kijiji na mtaa.
Hatua hii inaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha utawala wa sheria, haki na usawa wa kijamii, kwa kuhakikisha mwananchi hapati tabu kupata msaada wa kisheria, bila kujali eneo alipo.
Ends...








0 Comments