TATO YAIMARISHA ULIPAJI KODI SEKTA YA UTALII KUPITIA MAFUNZO MAALUM YA TRA
Na Joseph Ngilisho – Arusha
CHAMA cha Waendeshaji wa Utalii Tanzania (TATO) kimechukua hatua madhubuti katika kuimarisha ulipaji wa kodi na usimamizi wa mapato katika sekta ya utalii, baada ya zaidi ya wanachama 200 kushiriki mafunzo maalum yaliyoandaliwa na kuendeshwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yakilenga matumizi ya Mfumo Jumuishi wa Kidijitali wa Kodi za Ndani (PRI).
Mafunzo hayo yaliyofanyika leo januari 28,2026 katika Hoteli ya Gran Meliá jijini Arusha, yalilenga kuwawezesha wadau wa sekta ya utalii kuelewa kwa kina mabadiliko ya mifumo ya kodi, kuongeza uwazi na ufanisi katika ulipaji wa kodi, pamoja na kuimarisha ushiriki wa walipa kodi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TATO, Elirehema Maturo, alisema kuwa TATO inaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali kupitia TRA ili kuhakikisha wanachama wake wanakuwa na uelewa wa kutosha juu ya mifumo mipya ya kidijitali, kwa lengo la kulinda maslahi ya wafanyabiashara na kuchangia maendeleo ya Taifa.
“Sekta ya utalii ni mhimili muhimu wa uchumi wa Taifa. Mafunzo haya yanahakikisha kuwa mabadiliko ya sera na mifumo ya kodi yanaeleweka vyema na kutekelezwa kwa ufanisi bila kuathiri ukuaji wa biashara,” alisema Maturo.
Alifafanua kuwa Mfumo wa PRI unalenga kuondoa changamoto za makadirio yasiyo sahihi ya kodi kwa kutumia taarifa halisia za biashara, sambamba na kupunguza mwingiliano wa ana kwa ana kati ya mlipa kodi na mkusanya kodi, hatua inayoongeza uwazi, uaminifu na uwajibikaji.
Maturo alisisitiza kuwa sekta ya utalii ina mnyororo mpana wa thamani unaohusisha waendeshaji wa safari, hoteli, mawakala wa usafiri pamoja na wasambazaji wa bidhaa na huduma mbalimbali, hivyo ni wajibu wa kila mdau kutimiza kikamilifu wajibu wake wa kisheria katika kuchangia mapato ya Taifa.
Kwa upande wake, Meneja wa Ritani kutoka Divisheni ya Walipa Kodi Mkoa wa Kati (GnMTD), Sunday Kayombo, alisema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa TRA wa kutoa elimu kwa walipa kodi mara baada ya uzinduzi rasmi wa Mfumo Jumuishi wa Kodi za Ndani uliofanywa na Kamishna wa Kodi za Ndani.
Kayombo alisema mfumo huo umebuniwa kurahisisha na kuboresha ulipaji wa kodi kwa kuwawezesha walipa kodi kupata huduma kwa saa 24 bila ulazima wa kufika katika ofisi za TRA kwa huduma nyingi ambazo awali zilihitaji uwepo wa ana kwa ana.
“Mfumo huu umezingatia makundi yote ya walipa kodi na umejumuisha moduli mbalimbali zitakazoanza kufanya kazi mara baada ya kuanza rasmi kwa matumizi yake,” alisema.
Aliongeza kuwa TRA imejipanga kuhakikisha elimu hiyo inawafikia walipa kodi wote kupitia mafunzo ya ana kwa ana, majukwaa ya mtandaoni na huduma maalum za uwezeshaji zinazotolewa katika ofisi zote za TRA nchini.
Kwa mujibu wa Kayombo, walipa kodi wanaweza kupata msaada kwa kufika katika ofisi za TRA zilizo karibu, ambako watumishi waliopatiwa mafunzo maalum wako tayari kusaidia usajili na kutoa maelekezo ya matumizi sahihi ya mfumo huo, unaopatikana kupitia simu janja, kompyuta mpakato na vifaa vyote vinavyounganishwa na intaneti.
TRA pia ilibainisha kuwa mfumo huo umeunganishwa na taasisi zaidi ya 60 za Serikali, zikiwemo TANAPA, NCAA na TAWA, jambo linalorahisisha utambuzi wa malipo yote yanayofanywa kama gharama halali za biashara kupitia Mfumo wa TIR.
Kwa mujibu wa TATO, utekelezaji wa Mfumo wa PRI unatarajiwa kuongeza ushindani wa haki katika sekta ya utalii, kuimarisha mahusiano kati ya walipa kodi na TRA, pamoja na kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika pato la Taifa na maendeleo ya kiuchumi ya nchi.
Ends..










0 Comments