LHRC YAIBURUZA SERIKALI MAHAKAMA YA AFRIKA MASHARIKI KUPINGA KUFUNGA MTANDAO NCHINI


LHRC YAFUNGUA KESI MAHAKAMA YA AFRIKA MASHARIKI KUPINGA KUFUNGA MTANDAO NCHINI


Na Joseph Ngilisho-ARUSHA


Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimewasilisha Kesi Na. 56/2025 katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki, kikipinga kitendo cha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuzima huduma za mtandao kwa siku sita kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 4, 2025.


Kwa mujibu wa maelezo yaliyowasilishwa mahakamani, LHRC inadai kuwa mnamo Oktoba 29, 2025 majira ya saa tano asubuhi, huduma za mtandao nchini zilikatika ghafla na kuathiri maeneo yote ya Tanzania. Huduma hizo zilirudi katika hali ya kawaida Novemba 4, 2025, na tayari zilikuwa zimesababisha madhara makubwa ya kijamii, kiuchumi na kiutawala.


LHRC imeeleza kuwa zuio hilo lilibana upatikanaji wa taarifa muhimu kwa wananchi, likahujumu mawasiliano na shughuli za kiuchumi ikiwemo huduma za kibenki mtandaoni, biashara za kimtandao na upatikanaji wa huduma za afya kwa njia ya kidijitali. Kituo hicho kimedai kuwa hasara zilizotokana na usumbufu huo zimetajwa kufikia mamilioni ya shilingi.


Aidha, zuio hilo lilitokea kipindi nyeti cha uchaguzi, na hivyo kuwanyima wananchi fursa ya kupata taarifa muhimu kuhusu usalama na mwenendo wa mchakato wa kupiga kura. Ingawa Serikali ilieleza kuwa hatua hiyo ililenga kuzuia vurugu, LHRC inasema sababu hizo hazikidhi misingi ya demokrasia, hazikufuata utaratibu wa kisheria na hazikuwa na uhalali wa kutosha kuhalalisha hatua hiyo nzito kwa taifa.


Katika maombi yake, LHRC limeiomba Mahakama ya Afrika Mashariki kutamka kuwa hatua ya kuzimwa kwa mtandao ilikiuka vifungu 6(d), 7(2) na 8(1)(c) vya Mkataba wa Kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki wa mwaka 1999, ambavyo vinaitaka nchi mwanachama kutii misingi ya utawala bora, haki za binadamu na uwajibikaji.


Kituo hicho pia kinataka Mahakama itoe maelekezo yatakayozuia Serikali ya Tanzania kurudia kuzima mtandao bila msingi wa kisheria, bila sheria maalum inayoruhusu kufanya hivyo au bila amri ya mahakama.


Inatarajiwa kuwa baada ya kupokea ilani ya kufunguliwa kwa shauri hilo kutoka kwa Msajili wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki, Mwanasheria Mkuu wa Tanzania atawasilisha majibu yake ndani ya siku 45 kama inavyotakiwa na taratibu za kimahakama.


— Mwisho

Post a Comment

0 Comments