By Arushadigital -Dar
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es salaam imeombwa kutoa amri ya kupewa dhamana ama kufikishwa Mahakamani kwa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Geofrey Mwambe.
Maombi hayo ya dhamana yamefunguliwa kupitia hati ya dharura na Wakili wa Mwambe, Hekima Mwasipu yenye namba 289778 ya mwaka 2025 dhidi ya wajibu maombi watatu Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na ZCO wa Kanda ya Dar es Salaam.
Katika hati hiyo, Wakili Mwasipu anadai kuwa Mwambe ameshikiliwa kwa zaidi ya siku nne katika Kituo cha Polisi Kigamboni bila kupewa dhamana ya polisi wala kufikishwa mahakamani kama sheria inavyoelekeza.
Wakili Mwasipu ameiomba mahakama kusikiliza maombi hayo haraka iwezekanavyo, huku akisisitiza kuwa kuchelewesha kutasababisha kuendelea kukiukwa kwa haki za msingi za mwombaji.
Aidha katika maelezo yake, Mwasipu anadai kuwa familia ilimpelekea chakula Kituo cha Polisi Kigamboni alipokuwa amehifadhiwa tangu Disemba 7, 2025 lakini wakajibiwa na Askari Polisi kuwa hayupo kituoni hapo.
“Tumewafungua maombi ya kuomba Mwambe apewe dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa sababu ameshikiliwa kwa zaidi ya siku nne kinyume na sheria ni wajibu wa Jeshi la Polisii wanaomshikilia kumuachia kwa dhamana na wakiona kuna sababu za kuendelea kumshikilia kwa zaidi ya saa 24.
Alisema sheria inasema wanatakiwa kupeleka maombi mahakamani kuomba ruhusa ya mahakama waendelee kumshikilia zaidi ya masaa 24 mpaka sasa hivi hilo halijafanyika, familia inahangaika kutafuta ndugu yao alipo lakini juhudi hazijazaa matunda.
“Sababu za kukamatwa ni uchochezi na aliniambia mimi kama Wakili wake na alihojiwa kuhusu huo uchochezi lakini hakupewa dhamana, na alikamatwa nyumbani kwake saa nane usiku,”. Wakili Hekima Mwasipu.
Ends .

0 Comments