By Arushadigital-DODOMA
Waziri wa Zamani Jenistar Mhagama Afariki Dunia Leo Mbunge wa Peramiho, Jenista Joakim Mhagama, amefariki dunia leo 11 Desemba 2025 jijini Dodoma. Taarifa hiyo imetolewa na Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Azzan Zungu, ambaye ameeleza kuwa Bunge limepokea msiba huo kwa masikitiko makubwa.
Spika ametuma salamu za pole kwa Wabunge, familia, ndugu, jamaa pamoja na wananchi wa Jimbo la Peramiho. Ameomba Mungu awape nguvu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu na kusema mipango ya mazishi itatolewa na Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na familia.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema amesikitishwa na taarifa ya kifo Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Mhe. Jenista Mhagama kilichotokea Desemba 11, 2025 jijini Dodoma.
Kupitia kwenye mtandao wake wa Instagram, Rais Samia amepakia taarifa inayosomeka "Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama, ninatoa pole kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, wananchi wa Jimbo la Peramiho, familia, ndugu, jamaa na marafiki"
Kwenye Taarifa ya Rais Samia imeeleza kuwa kwa miaka 38, Mhe. Mhagama amekuwa mwanachama mahiri wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kiongozi wa vijana, kiongozi wa wanawake, waziri katika awamu mbalimbali na mnasihi wa wengi katika siasa na maisha.


0 Comments