Na Joseph Ngilisho – ARUMERU
DIWANI wa Kata ya Olorien katika Halmashauri ya Arusha, Hendri Sikoi, ameipongeza Serikali kwa kuipatia kata hiyo mradi wa ujenzi wa miundombinu katika Shule ya Msingi Mringa unaogharimu shilingi milioni 150, huku akitaka kasi ya utekelezaji iongezwe ili mradi ukamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
Sikoi alitoa kauli hiyo leo desemba 8,2025 wakati wa ziara yake ya ukaguzi shuleni hapo, ziara iliyoshirikisha Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC), wataalamu wa sekta ya ujenzi pamoja na maafisa elimu.
Akizungumza baada ya kukagua hatua za awali za ujenzi, Diwani Sikoi alisema mradi huo ni mkombozi mkubwa kwa wanafunzi na jamii ya Mringa kutokana na changamoto za muda mrefu za upungufu wa madarasa na matundu ya vyoo.
>
“Serikali imetupa uwekezaji mkubwa wa shilingi milioni 150. Hii ni fedha nyingi na ni uwekezaji muhimu kwa watoto wetu. Tunatarajia kuona mazingira bora ya kujifunzia mwakani, kwani madarasa na vyoo vilivyokuwa kero sasa vinajengwa kwa ubora unaotakiwa,” alisema.
Aidha, alimwelekeza mhandisi wa Wilaya na kamati ya ujenzi kuongeza kasi ya ujenzi ili kukidhi matarajio ya wananchi.
>“Kwa thamani ya shilingi milioni 150 tulipaswa kuwa mbali zaidi. Tumetoa maelekezo kwa mhandisi kusimama karibu na mradi huu. Tunataka matokeo halisi na ukamilishaji kwa wakati,” alisisitiza Sikoi.
Katika ziara hiyo, Sikoi aliwataka wahandisi wa Wilaya kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye miradi ya maendeleo, hususan ile inayogharimiwa na fedha za Serikali Kuu chini ya Rais, ili kuhakikisha ubora na matumizi sahihi ya fedha za umma vinazingatiwa.
Alipongeza pia Kamati ya Maendeleo ya Kata kwa ushirikiano waliompa wakati wa ukaguzi huo, akisema umoja wao ndiyo msingi wa usimamizi imara wa miradi.
>
“WDC wamefanya kazi nzuri. Ziara hii imetupa nafasi ya kuona hatua zilizofikiwa na kutoa maelekezo kabla changamoto hazijawa kubwa,” alisema.
Akizungumzia changamoto za kata hiyo, Sikoi alisema bado wanakabiliwa na masuala ya barabara, mafuriko na mazingira. Hata hivyo, alibainisha kuwa wananchi kwa kushirikiana na viongozi wa vitongoji wameanza kuchangia nguvu kazi kwa ujenzi wa mitaro na shughuli zinazotatua changamoto hizo.
Aidha, alisifu kasi ya miradi inayotekelezwa na Mbunge wa jimbo hilo pamoja na Serikali ya Rais, akisema utekelezaji wa Ilani ya CCM unakwenda vizuri kuelekea 2025.
>
“Nawaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano. Serikali imeshafanya kazi kubwa. Sisi viongozi lazima tusimame kidete kuhakikisha manufaa yanawafikia wananchi,” alihitimisha.
Mtendaji wa Kata ya Olorien, Charles Sikoi, alisema mradi unaendelea vizuri licha ya hitaji la kuongeza kasi ili kufikia muda wa ukamilishaji kama ilivyoelekezwa na Mkurugenzi wa Halmashauri.
>
“Tumeridhishwa na hatua za awali, lakini tumeagiza kasi iongezwe. Tunampongeza Diwani kwa kufuatilia miradi kwa ukaribu na kuhamasisha maendeleo; kasi yake inaimarisha kata yetu,” alisema.
Katika kikao kazi cha WDC, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Olosiva, Jonas Kimati, alisema wananchi wamekuwa wakikumbwa na kero ya vibaka na kwamba wameomba suala hilo lifikishwe katika Baraza la Madiwani ili lipatiwe ufumbuzi wa kudumu.
>
“Vibaka wamekuwa kero kubwa kwa wakazi wa Olosiva. Tunaomba hatua zichukuliwe ili wananchi waishi kwa amani,” alisema.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni,Miundombinu duni ya barabara,Ukosefu wa ajira kwa vijana,Kuongezeka kwa utegemezi na vitendo vya uhalifu
Kimati alisema wana imani kwamba uongozi wa kata utaendelea kushirikiana na halmashauri kutafuta suluhu ya changamoto hizo.
Viongozi wa kata walihakikisha kuwa maoni yote yatafikishwa kwenye vikao husika na kufanyiwa kazi haraka, sambamba na usimamizi wa karibu wa mradi wa Shule ya Msingi Mringa hadi ukamilike.
Ends..







0 Comments