RC MAKALLA AZINDUA USIKILIZAJI KERO ZA MADEREVA BAJAJI NA BODABODA ARUSHA

 RC MAKALLA AZINDUA USIKILIZAJI KERO ZA MADEREVA BAJAJI NA BODABODA ARUSHA

Aaahidi kuyafikia makundi yote ya kijamii na kusikiliza kero za wananchi

Na Joseph Ngilisho– Arusha
 



Mkuu wa Mkoa wa Arusha,  CPA   Makalla, amesema kusikiliza na kutatua kero za wananchi kutakuwa kipaumbele chake katika utumishi wake mkoani humo, huku akiahidi kuwafikia wananchi wa makundi yote bila ubaguzi.

Kauli hiyo aliitoa leo Jumatatu, Desemba 15, 2025, alipofungua na kuongoza kikao maalumu cha kusikiliza kero na changamoto za madereva wa bodaboda na bajaji wa Mkoa wa Arusha, kilichofanyika katika viwanja vya Makumbusho ya Azimio la Arusha.



Akizungumza katika salamu zake za utangulizi,  Makalla aliyekuwa ameambatana na Wakuu wote wa Wilaya za Mkoa wa Arusha, alisema mtazamo wake wa kiuongozi ni kuhakikisha Serikali inawakaribia wananchi badala ya wananchi kuisubiri Serikali, kwa lengo la kutatua changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za kila siku.

Alisisitiza kuwa kusikiliza kero za wananchi kutakuwa utamaduni wa kudumu katika uongozi wake, akieleza kuwa makundi ya wajasiriamali wadogo, yakiwemo ya bodaboda na bajaji, yana mchango mkubwa katika uchumi wa Mkoa na hivyo yanapaswa kusikilizwa na kushughulikiwa changamoto zao kwa wakati.

Aidha, Makalla aliwaagiza Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanafanya ziara za mara kwa mara katika maeneo yao ya utawala kwa lengo la kuwatembelea wananchi, kusikiliza kero zao na kuzitatua kwa kushirikiana na mamlaka husika, badala ya kusubiri malalamiko kufika ngazi ya juu.

Kikao hicho kililenga kutoa fursa kwa madereva wa bodaboda na bajaji kueleza changamoto zinazowakabili, ikiwemo masuala ya usalama, tozo, miundombinu na mahusiano yao na vyombo vya dola, huku Serikali ya Mkoa ikiahidi kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na taasisi zinazohusika.

Kwa upande wao, madereva wa bodaboda na bajaji waliipongeza Serikali ya Mkoa kwa kuandaa kikao hicho, wakieleza kuwa ni mara chache kupata fursa ya kukutana moja kwa moja na uongozi wa juu kusikilizwa kero zao.

Mmoja wa viongozi wa bodaboda Mkoa wa Arusha alisema changamoto kubwa zinazowakabili ni pamoja na tozo wanazodai kuwa ni nyingi, ukosefu wa maeneo rasmi ya kupakia abiria pamoja na changamoto za usalama barabarani.

“Tunaishukuru Serikali kwa kutusikiliza. Kero zetu ni nyingi, lakini tunaamini kikao hiki kitakuwa mwanzo wa suluhisho, hasa kwenye suala la tozo na maeneo ya kazi,” alisema.

Naye mwakilishi wa madereva wa bajaji alisema changamoto zao zimekuwa zikihusisha ukamataji wa mara kwa mara, faini kubwa na ukosefu wa elimu ya mara kwa mara ya sheria za usalama barabarani.

“Tunaomba elimu itolewe zaidi na sheria zitumike kwa haki. Sisi ni vijana tunaotafuta riziki halali,” alisema.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, Serikali ya Mkoa itazifanyia kazi kero zote zilizowasilishwa kwa kushirikiana na Halmashauri, Jeshi la Polisi na taasisi nyingine husika, huku akiahidi kuwa vikao kama hivyo vitaendelea kufanyika mara kwa mara ili kujenga mawasiliano ya karibu kati ya Serikali na wananchi.

Ends..

Post a Comment

0 Comments