DIWANI ENYASI AANZA KWA KISHINDO SINONI AWEKA MKAKATI MPYA WA KIUTENDAJI, AAHIDI UWAJIBIKAJI NA USHIRIKISHWAJI WA WANANCHI

 DIWANI ENYASI AWEKA MKAKATI MPYA SINONI, AAHIDI UWAJIBIKAJI NA USHIRIKISHWAJI WA WANANCHI

Na Joseph Ngilisho- ARUSHA 



DIWANI wa Kata ya Sinoni mkoani Arusha, Mheshimiwa Peter Enyasi, amesema amejiandaa kuiongoza kata hiyo kwa mkakati unaozingatia uwajibikaji, ushirikishwaji wa wananchi na utendaji wa karibu, akisisitiza kuwa mshikamano wa viongozi na wananchi ndio msingi wa maendeleo ya haraka na endelevu.


Akieleza namna alivyojipanga kiutendaji leo jumatatu desemba 15 ,2025 wakati akiongea na kamati ya maendeleo ya kata (WDC), Diwani Enyasi alisema kuwa “nimejipanga kufanya kazi kwa karibu na viongozi wa ngazi zote kuanzia wenyeviti wa mitaa, watendaji wa kata hadi taasisi za serikali, ili mipango ya maendeleo ipangwe na kutekelezwa kwa uwazi na kwa maslahi ya wananchi wote.”Aliongeza kuwa uongozi wake utaongozwa na misingi ya uwajibikaji na utendaji unaopimika.


Mara baada ya kuingia rasmi ofisini tarehe 15 Desemba 2025, Diwani Enyasi alimuelekeza Mtendaji wa Kata kuandaa muhtasari wa mahitaji muhimu ya ofisi utakaowasilishwa Halmashauri, ikiwemo meza na viti, kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi.


 Alieleza kuwa “utendaji bora unaanzia kwenye ofisi zenye mazingira rafiki kwa watumishi na wananchi wanaohitaji huduma.”


Aidha, alibainisha kuwa mkakati wake unahusisha kushuka kwa wananchi kwa kufanya vikao vya wazi katika kila mtaa, kusikiliza changamoto zao na kutoa mrejesho wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo. Kwa mujibu wake, “nataka uongozi wangu uwe wa karibu na wananchi, nisikilize kero zao na nirejee kuwaeleza hatua zilizochukuliwa.”


Katika kuimarisha usalama na uwajibikaji, Diwani Enyasi alizitaka taasisi zote za serikali zilizopo ndani ya kata kufunga kamera za ulinzi (CCTV), akisema hatua hiyo itasaidia kufuatilia matukio mbalimbali yanapotokea.


 Alitolea mfano maandamano ya tarehe 29, akisema “kamera zitasaidia kupata ukweli wa matukio na pia kuboresha namna wananchi wanavyohudumiwa katika ofisi za umma.”


Akigusia maadili ya uongozi, Diwani huyo alikemea vikali vitendo vya rushwa, akisisitiza kuwa havina nafasi katika maendeleo ya Kata ya Sinoni. Alisema “rushwa ni adui wa maendeleo; tunahitaji ushiriki wa wadau kwa uadilifu na bila mianya ya rushwa.”


Kwa upande wa vijana, Diwani Enyasi alisema mkakati wake ni kuhakikisha kila mtaa unakuwa na timu za mpira na michezo mbalimbali ili kuwajumuisha vijana, hususan wanaojiita Gen Z, katika shughuli chanya. Alibainisha kuwa “ni jambo la kushangaza kuona Jiji la Arusha linakosa timu imara ya mpira wa miguu wakati serikali imewekeza fedha nyingi kwenye ujenzi wa viwanja.”


Mwisho, aliwataka wenyeviti wote wa mitaa kuandaa dira za maendeleo zitakazobainisha maono na vipaumbele vya wananchi wao, akisisitiza kuwa “dira hizo zitakuwa msingi wa kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo kwa maslahi ya wananchi wa Kata ya Sinoni.”






Post a Comment

0 Comments