JAFO AWAHAMASISHA WATUMISHI KISARAWE: WELEDI, UBUNIFU NA USHIRIKIANO NDIO NGUZO YA MAENDELEO

JAFO AWAHAMASISHA WATUMISHI KISARAWE: WELEDI, UBUNIFU NA USHIRIKIANO NDIO NGUZO YA MAENDELEO

Na Alex Sonna, Kisarawe

Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, Dkt. Selemani Jafo, amewataka watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe kuongeza weledi, bidii na mshikamano katika utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya watumishi wa Serikali na Baraza la Madiwani ni msingi muhimu wa kuharakisha maendeleo ya wilaya hiyo na kuboresha huduma kwa wananchi.


Dkt. Jafo ametoa wito huo wakati wa kikao chake na watumishi wa halmashauri hiyo, akieleza kuwa lengo la mkutano huo lilikuwa ni kuwashukuru kwa kazi wanazozifanya, pamoja na kuwahamasisha kuendeleza ari ya kufanya kazi kwa moyo mmoja katika kuwatumikia wananchi wa Kisarawe.

Amesisitiza kuwa utendaji wa kazi kwa kujituma na uaminifu ni wajibu wa kila mtumishi wa umma, akiwakumbusha kuwa nafasi walizonazo ni fursa adimu kwa kuzingatia changamoto ya ajira nchini. 


“Ni muhimu kupendana na kushirikiana kama watumishi wa Serikali. Fanyeni kazi bila kuchoka, kwa kuwa mnalipwa mshahara wakati wapo wananchi wengi bado hawana ajira. Fanyeni kazi kama ibada; mkifanya hivyo kwa moyo wote mtapata mafanikio makubwa,” amesema.


Aidha, amewataka watumishi kujiepusha na utendaji wa mazoea na badala yake wawe wabunifu, wawajibikaji na wenye maono, ili kuacha alama chanya katika maeneo wanayoyahudumia na kujenga imani ya wananchi kwa Serikali yao.


Katika hatua nyingine, Mbunge huyo amesisitiza umuhimu wa kutafuta na kusimamia vyanzo mbalimbali vya mapato pamoja na kuhakikisha matumizi sahihi ya fedha za miradi ya maendeleo, akibainisha kuwa usimamizi bora wa rasilimali ndio unaoweza kuhakikisha miradi inaleta tija na kugusa maisha ya wananchi moja kwa moja.


Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Nyahori Mahumbwe, ameahidi kutoa ushirikiano wa karibu kwa Mbunge huyo pamoja na viongozi wengine, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki na ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi zinatekelezwa ipasavyo.


 “Tupo tayari kufanya kazi mchana na usiku kuwatumikia wananchi na kutekeleza ahadi mlizozitoa wakati wa uchaguzi. Watekelezaji wa mkataba ule ni sisi watumishi wa Serikali, hivyo tutahakikisha tunashirikiana kikamilifu kutekeleza Ilani ya Uchaguzi,” amesema.


Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kisarawe, Aidan Kitare, amesema Baraza la Madiwani lipo tayari kufanya kazi kwa mshikamano na weledi katika kipindi cha miaka mitano ijayo, akiahidi kusimamia maslahi ya wananchi na kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa usawa katika maeneo yote ya wilaya hiyo.




-Ends..

Post a Comment

0 Comments