MWANAFUNZI DARASA LA SABA AJINYONGA KITUO CHA WATOTO YATIMA ARUMERU
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Mwanafunzi wa darasa la saba aliyefahamika kwa jina la Ibrahim Elibariki (15), anayelelewa katika Kituo cha Watoto Yatima cha FRUIT ORPHANAGE kilichopo Kata ya Ambureni, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia tai ya shule aliyokuwa amevaa kituoni hapo.
Kituo hicho cha watoto yatima kinamilikiwa Mkurugenzi ISACK SUKARI,ambaye amekuwa akihudumia na kulea watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa walezi wa kituo hicho, tukio hilo la kusikitisha lilitokea asubuhi wakati watoto waliokuwa kituoni hapo wakijiandaa kwenda shuleni kama ilivyo kawaida yao.
Akizungumza na waandishi wa habari, mlezi wa kituo hicho alisema mwanafunzi huyo aliamka mapema pamoja na wenzake, akanywa chai na kujiandaa kwenda shuleni kama kawaida. Hata hivyo, ilibainika baadaye kuwa hakuelekea shuleni pamoja na wenzake bali alizunguka nyuma ya eneo la makazi yao.
“Marehemu aliamka vizuri tu asubuhi, alikunywa chai na wenzake na kujiandaa kwenda shuleni.
Lakini baada ya muda tuligundua kuwa alizunguka nyuma ya nyumba ambako alichukua tai yake ya shule aliyokuwa amevaa na kujitundika kwenye paa la nyumba,” alisema mlezi huyo.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kabla ya kuchukua hatua hiyo, mwanafunzi huyo alichomeka madaftari yake kwenye paa la nyumba, hali inayodhaniwa kuwa alifanya akiwa peke yake bila kugunduliwa na wenzake.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ambureni, Olais Mollel, alisema alipokea taarifa za tukio hilo kutoka kwa wakazi wa eneo hilo na kufika katika kituo hicho kushuhudia hali halisi kabla ya kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi.
“Nilipigiwa simu na kuambiwa kuhusu tukio hilo. Nilifika eneo la tukio na baadaye tukawasiliana na Jeshi la Polisi ambao walifika na kuuchukua mwili wa marehemu kwa ajili ya kuuhifadhi katika chumba cha kuhifadhia maiti (mochwari) huku uchunguzi zaidi ukiendelea,” alisema Mollel.
Jeshi la Polisi mkoani Arusha linaendelea na uchunguzi kubaini chanzo na mazingira halisi yaliyopelekea mwanafunzi huyo kufikia uamuzi huo.
Tukio hilo limeacha huzuni kubwa kwa watoto wanaolelewa katika kituo hicho pamoja na wakazi wa Kata ya Ambureni, huku baadhi wakitoa wito kwa jamii kuongeza uangalizi na msaada wa kisaikolojia kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili kuwasaidia kukabiliana na changamoto za maisha.
Ends..

0 Comments