Nguyaine afungua ‘vita’ ya Sh6m Marya
..Awashtaki Kadogoo, Kalanga; wazee wampa kibali cha ‘kupasua chungu’
Na Joseph Ngilisho | MONDULI
ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Efraimu Nguyaine, ameifikisha katika Baraza Kuu la Kimila la Maa (Marya) kesi ya kudai Sh milioni sita, akiwataka viongozi wawili aliowataja kuwa walimshawishi kutoa fedha hizo kwa ajili ya shughuli za halmashauri.
Nguyaine amewataja Mbunge wa Monduli, Isack Kadogoo, na Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Julius Kalanga, akidai walihusika katika mchakato uliomfanya kutoa fedha hizo wakati wakihudumu katika Halmashauri ya Monduli.
Kwa mujibu wa Nguyaine, Kadogoo alitoa Sh milioni nne, huku yeye akiombwa kuchangia Sh milioni sita ili kukamilisha shughuli za halmashauri, akieleza kuwa alifanya hivyo kwa matarajio ya kurejeshewa fedha hizo baadaye.
Amesema viongozi hao waliitwa mbele ya Marya ili kusikiliza shauri hilo, lakini hawakufika.
“Mimi sikutaka kikao, nilichokuwa nataka ni kurejeshewa fedha zangu. Walipoitwa hawakuitikia, ndiyo maana suala hili limefika hapa,” amesema Nguyaine.
Kalanga: Ananidai nini?
Akizungumza kuhusu madai hayo, Kalanga amesema hana taarifa za kina kuhusu shauri hilo na kumtaka Nguyaine kuweka wazi anachodai kutoka kwake.
“Mtafute yeye ajue ananidai nini. Anawezaje kudai watu wawili?” amesema Kalanga.
Marya yamruhusu ‘kupasua chungu’
Katika hatua nyingine, kwa mujibu wa hati iliyoonekana, Baraza la Marya limempa Nguyaine kibali cha kutekeleza utaratibu wa kimila unaojulikana kama ‘kupasua chungu’, kuanzia Agosti 6 hadi Oktoba 30, 2026.
Hatua hiyo imekuja baada ya mchakato wa shauri hilo kufikishwa katika baraza hilo, huku Nguyaine akisisitiza kuwa lengo lake ni kurejeshewa fedha anazodai alizitoa.
Mzee mmoja wa kimila amesema Marya ni ngazi ya juu ya utatuzi wa migogoro katika mfumo wa kimila wa Wamaasai, akieleza kuwa utaratibu huo unaweza kufuatwa baada ya hatua za upatanishi kushindikana.
Jitihada za kumpata Kadogoo ili kutoa upande wake kuhusu madai hayo ,alisema hana taarifa za kudaiwa kiasi hicho cha fedha wala hakumbuki kama kunadeni la aina hiyo.
"Mimi sijui kama nadaiwa muulizeni vizuri hilo deni ni la lini na kuhusu nini???".Alihoji Kadogoo Kwa njia ya Simu
Hata hivyo, madai ya Nguyaine dhidi ya viongozi hao bado ni madai yanayohitaji majibu ya pande zote, hasa kuhusu mazingira ya kutolewa kwa fedha hizo na kama kulikuwa na makubaliano ya kurejeshwa kwake.
Ends


Post a Comment