Breaking🔥

MAELFU WAFURIKA KUTABARUKU KANISA KUU LA MT. TERESIA ARUSHA

MAELFU WAFURIKA KUTABARUKU KANISA KUU LA MT. TERESIA ARUSHA

Jengo la Sh7.6 bilioni lakamilika baada ya miaka 15; viongozi wataka liwe kitovu cha imani, umoja na huduma kwa jamii

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

MAELFU ya waamini wa Kanisa Katoliki wamefurika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu, Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, kushuhudia Misa Takatifu ya kutabaruku jengo hilo lililogharimu Sh7.6 bilioni baada ya ujenzi wa miaka 15.

Misa hiyo ya kihistoria imewakutanisha waamini kutoka maeneo mbalimbali nchini pamoja na wageni waalikwa, akiwamo Majaji, Maaskofu, viongozi wa Serikali, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa taasisi mbalimbali mkoani Arusha.

Ibada hiyo imeongozwa na Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa, huku viongozi wa Kanisa wakisisitiza kuwa Kanisa Kuu hilo si alama ya mafanikio ya ujenzi wa jengo pekee, bali ni kituo cha imani, umoja, matumaini na huduma kwa Mungu na jamii.

Akizungumza Agosti 7,2026 katika sherehe hizo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha, Isaac Amani, alisema kuwekwa wakfu kwa Kanisa hilo ni hatua muhimu katika historia ya Jimbo, huku akiwataka waamini kulitumia kama kituo cha kujenga imani na kuimarisha utumishi kwa Mungu na jamii.

Alisema jengo hilo limejengwa kwa ajili ya ibada na linapaswa kuwa urithi wa kiroho utakaowanufaisha waamini na vizazi vijavyo.

“Tumejenga nyumba hii kwa ajili ya ibada na sasa tunaomba Mungu aibariki, ili itumike katika mahubiri na iwe nyumba ambayo kwa vizazi vijavyo watu watakuja hapa na kumkumbuka Mungu,” alisema.

Askofu Amani alisema kuwekwa wakfu kwa Kanisa hakumaanishi kutengwa kwa jengo pekee, bali ni mwito kwa waamini wenyewe kuishi maisha yanayolingana na imani yao.

Alisema Wakristo huanza safari yao ya imani kupitia ubatizo, ambao ni ishara ya kuingizwa katika familia ya Mungu na Kanisa, hivyo kila muamini anapaswa kuwa shahidi wa imani yake katika jamii.

AMANI AWATAKA VIJANA KUSHIRIKISHWA

Katika hatua nyingine, Askofu Amani alisema Kanisa na jamii zinapaswa kuwapa vijana nafasi zaidi ya kushiriki katika maamuzi yanayohusu maisha yao na mustakabali wa jamii.

Alisema vijana wamekuwa wakitoa ujumbe wa kutaka kusikilizwa na kushirikishwa zaidi katika kupanga na kufanya maamuzi, akisisitiza kuwa sauti yao haipaswi kupuuzwa.

Alisema katika mkutano wa maaskofu wa Afrika Mashariki uliofanyika Nairobi, Kenya, vijana walisisitiza haja ya kujenga maridhiano, matumaini, haki, utawala bora na ushiriki wao katika jamii.

“Tuwasikilize changamoto zao, tuwape mwongozo na mashauri ya maisha ya imani na jamii, tukionesha kwa matendo kwamba tunawajali. Sio kwa maneno tu, bali kwa matendo,” alisema.

Alisema Kanisa linapaswa kuwa karibu na vijana, kuwasikiliza na kuwashirikisha katika masuala ya maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ili kuwaandaa kuwa viongozi na wazazi bora wa vizazi vijavyo.

MLOLA: KANISA KUU NI KITOVU CHA UMOJA

Kwa upande wake, Askofu Gilbert Mlola, akitoa salamu kwa niaba ya Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na maaskofu wengine, aliwapongeza waamini wa Jimbo Kuu la Arusha kwa kukamilisha ujenzi wa Kanisa hilo.

Alisema Kanisa Kuu si jengo la kawaida, bali ni alama ya mamlaka ya kichungaji ya Askofu, kitovu cha umoja wa waamini na mama wa makanisa yote katika Jimbo.

“Uwepo wa Kanisa Kuu la Jimbo ni ishara ya mamlaka ya kichungaji ya Askofu, kitovu cha umoja wa waamini wote wa Jimbo na chanzo cha maisha ya kiroho na kiutawala,” alisema.

Askofu Mlola alisema uzuri wa jengo hilo unapaswa kuwa ukumbusho kwamba Kanisa halijengwi kwa mawe na saruji pekee, bali pia na waamini ambao ni “mawe yaliyo hai” katika kujenga nyumba ya Mungu.

Aliwataka waamini kuendelea kushikamana na viongozi wao wa Kanisa, kudumisha umoja na upendo na kuimarisha uhusiano wao na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania pamoja na Baba Mtakatifu.

Akirejea mafundisho ya Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu, msimamizi wa Kanisa hilo, alisema upendo unapaswa kuwa kiini cha maisha ya Kanisa na kuwataka waamini kuufanya kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku.

Aidha, aliwapongeza maaskofu wakuu na maaskofu waliotangulia, mapadre na waamini wote kwa mchango wao katika kufanikisha ujenzi wa Kanisa hilo, akisema hatua hiyo ni ushahidi wa imani hai na mshikamano wa waamini.

TOBA: SERIKALI YATAMBUA MCHANGO WA KANISA

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Nguvila, alisema Serikali inautambua na kuuthamini mchango wa Kanisa Katoliki katika maendeleo ya jamii.

Dkt. Nguvila aliwapongeza viongozi wa Kanisa na waamini kwa jitihada zao za kukamilisha ujenzi wa Kanisa hilo, akisema mafanikio hayo yanaonyesha mshikamano, kujitolea na imani ya waamini.

“Kwa niaba ya Mkoa wa Arusha, tunawapongeza sana waamini na viongozi kwa jitihada kubwa mlizofanya katika ujenzi wa Kanisa hili. Mmefanya kazi nzuri na mmeweka historia njema,” alisema.

Alisema Kanisa Katoliki limekuwa mshirika muhimu wa Serikali katika kutoa huduma za msingi kwa wananchi, hususan katika sekta za elimu na afya.

Alisema kupitia shule, hospitali na taasisi nyingine, Kanisa limeendelea kusaidia Serikali kupunguza changamoto za upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

“Kanisa Katoliki limekuwa bega kwa bega na Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi, hasa katika maeneo ya afya na elimu. Ushirikiano huu ni muhimu kwa sababu unasaidia Serikali kuwafikia wananchi wengi zaidi,” alisema.

Dkt. Nguvila alisema Serikali ya Mkoa wa Arusha itaendelea kushirikiana na Kanisa Katoliki na taasisi nyingine za dini katika masuala yanayolenga kuboresha maisha ya wananchi na kuimarisha maendeleo.

Alisema milango ya Serikali ipo wazi kwa ushauri, ushirikiano na majadiliano na viongozi wa dini, akisisitiza kuwa maendeleo ya jamii yanahitaji nguvu za pamoja.

Aliongeza kuwa Serikali inatambua nafasi ya viongozi wa dini katika kuhamasisha amani, mshikamano, maadili na maendeleo ya jamii.

SHEREHE ZAWAKUTANISHA VIONGOZI

Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya siasa, Majaji, Maaskofu, viongozi wa dini na taasisi pamoja na maelfu ya waamini kutoka maeneo mbalimbali.

Ujenzi wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu umechukua takribani miaka 15 na kugharimu Sh7.6 bilioni, huku kukamilika kwake kukitajwa kuwa hatua kubwa katika historia ya Jimbo Kuu Katoliki la Arusha.

Kwa waamini, tukio hilo limekuwa zaidi ya sherehe ya kukamilika kwa jengo; limekuwa kilele cha miaka ya kujitolea, imani, michango na mshikamano katika kulijenga Kanisa ambalo sasa limewekwa wakfu kwa ajili ya ibada na huduma kwa vizazi vijavyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post