KKKT LOLIONDO KWAFUKUTA HAPAKALIKI WAUMINI WASALI NJE YA KANISA KWA WIKI NANE,MKUU WA JIMBO ATUHUMIWA ,ASKOFU MALASUSA ATAJWA,KATIBU MKUU AFUNGUKA

 Na Joseph Ngilisho | NGORONGORO

MGOGORO unaoendelea katika Kanisa la Kiinjili Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Loliondo, Jimbo la Maasai Kaskazini, umeingia katika hatua mpya baada ya Mamia ya waumini kuendelea kufanya ibada nje ya jengo la kanisa kwa zaidi ya wiki nane, wakipinga kuondolewa kwa mchungaji wao, Hery Johannes Lukumay, huku wakimwomba Askofu Mkuu wa KKKT, Dkt. Alex Malasusa, kuingilia kati kabla mgogoro huo haujasababisha mgawanyiko mkubwa zaidi ndani ya kanisa.

Waumini hao wanadai mchungaji huyo aliondolewa katika mazingira yenye utata bila wao kushirikishwa, wakisema hatua hiyo imeyumbisha huduma za kiroho, kugawa waumini na kuwalazimu kuendelea kuabudu nje ya kanisa huku wakisisitiza hawatarejea ndani ya jengo hilo hadi watakapopewa maelezo ya kina kuhusu sababu za kuondolewa kwake.


Mbali na kupinga uamuzi huo, waumini wanamshutumu Mkuu wa Jimbo la Maasai Kaskazini, Mchungaji Mathayo Loisaliye, kwa kile wanachodai ni uongozi usiozingatia ushirikishwaji na unaochochea migawanyiko, huku pia wakitoa madai ya matumizi yasiyo sahihi ya fedha na mali za kanisa. Madai hayo hayajathibitishwa na viongozi wanaotajwa.

Wakizungumza nje ya kanisa hilo leo Jumapili Agosti 2,2026, baadhi ya waumini walisema wamewasilisha malalamiko yao kwa viongozi wa dayosisi lakini hadi sasa hawajaona hatua zinazowaridhisha, wakisisitiza kuwa hawana imani na uongozi wa jimbo na wapo tayari kuhama usharika iwapo kiliochao kitaendelea kufumbiwa macho.

Mmoja wa waumini hao, Margaret Kileo, alisema kuendelea kwa mgogoro huo kunawaathiri hata watoto ambao hawapati mafundisho ya Sunday School kama ilivyokuwa awali.

"Tumekuwa tukisali nje kwa wiki nane. Tunataka ukweli ujulikane kuhusu kuondolewa kwa mchungaji wetu na tunahitaji viongozi wa kanisa watusikilize. Watoto hawapati mafundisho ya Sunday School kama ilivyokuwa awali na hali hii inaendelea kudhoofisha maisha ya kiroho ya usharika," alisema.

Naye muumini mwingine, Jonathan Tarimo, alisema hatua yao ya kuendelea kusali nje ya kanisa kwa zaidi ya wiki nane imetokana na kutoridhishwa na uamuzi wa uongozi wa jimbo kumuondoa mchungaji wao pamoja na madai ya matumizi yasiyo sahihi ya fedha na mali za kanisa wanayomwelekeza Mkuu wa Jimbo.

Tarimo alisema waumini wanataka uchunguzi huru ufanyike kuhusu tuhuma zilizotolewa dhidi ya mchungaji huyo na kwamba arejeshwe kazini ikiwa itabainika hakukuwa na kosa la kiutendaji, wakisisitiza kuwa alikuwa akisimamia uwajibikaji, uwazi na ulinzi wa mali za kanisa.

Waumini hao walisema iwapo mgogoro huo hautapatiwa ufumbuzi wa haraka, baadhi yao wako tayari kuhama usharika huo na kutafuta sehemu nyingine za kuabudu.

Kutokana na hali hiyo, wamemwomba Askofu Mkuu wa KKKT, Dkt. Alex Malasusa, kuingilia kati mgogoro huo wakidai juhudi za uongozi wa dayosisi hazijaleta suluhisho.

"Tunamuomba Askofu Mkuu atusikilize na atume timu huru kufanya uchunguzi ili haki itendeke kwa pande zote.

 Tunahitaji amani na umoja urejee kanisani," alisema mmoja wa waumini.

Hata hivyo, Mkuu wa Jimbo la Maasai Kaskazini, Mchungaji Mathayo Loisaliye, amevunja ukimya akisema hana mamlaka ya kuzungumzia mgogoro huo kwa kuwa tayari upo mikononi mwa Baba Askofu wa Dayosisi ambaye ndiye anayeshughulikia suala hilo.

Akizungumza kwa njia ya simu, Loisaliye alisema waumini waliowasilisha malalamiko dhidi yake tayari wamefikisha hoja zao kwa Baba Askofu na ameagizwa kutotoa kauli yoyote kuhusu mgogoro huo.

"Wamenitaja katika malalamiko yao, lakini jambo hilo linashughulikiwa na Baba Askofu ambaye ndiye mwajiri wangu. Nimeelekezwa nisilihusikie wala kulizungumzia kwa sasa," alisema.

Aliongeza kuwa Baba Askofu tayari amefanya ziara mbili Loliondo kufuatilia mgogoro huo na kwamba taarifa rasmi kuhusu chanzo cha mgogoro na hatua zinazochukuliwa zitatolewa na uongozi wa dayosisi.

"Naomba muwasiliane na Baba Askofu Godson Mollel kama mwajiri wangu. Sina majibu yoyote kuhusu jambo hili kwa sasa. Sitaki kulizungumzia wakati linaendelea kushughulikiwa na mamlaka husika," alisema.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati na msemaji wa dayosisi hiyo, Solomon Sambweti, amesema uongozi wa kanisa umeanza kushughulikia mgogoro huo na kwamba tayari mchungaji mpya amepatikana na anatarajiwa kuripoti muda wowote.

Akizungumza kwa njia ya simu, Sambweti alisema malalamiko ya waumini yamepokelewa na yanafanyiwa kazi kupitia Ofisi ya Askofu kwa mujibu wa taratibu za kanisa.

"Tumewasikia waumini na tunafanyia kazi hoja zao. Suala hili lipo chini ya Ofisi ya Askofu na linaendelea kushughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za kanisa," alisema.

Akijibu madai kuwa usharika huo umekaa muda mrefu bila mchungaji, Sambweti alisema tayari uongozi umemteua mchungaji mwingine.

"Tumeshampata mchungaji na ataripoti. Atakuwa pamoja na waumini wa Loliondo kuendelea na huduma," alisema.

Hata hivyo, alipohojiwa iwapo dayosisi imeunda tume maalumu ya kuchunguza mgogoro huo, alisema mchakato wote unasimamiwa na Ofisi ya Askofu bila kueleza hatua nyingine zinazoendelea.

Mgogoro huo unaendelea kuvuta hisia za waumini na viongozi wa kanisa, huku ukiibua hofu kuhusu mustakabali wa Usharika wa Loliondo na kuongeza shinikizo kwa uongozi wa juu wa KKKT kuharakisha suluhisho litakalorejesha utulivu, umoja na ibada za kawaida ndani ya usharika huo.






Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post