Breaking🔥

ALIYEIBIWA MAZULIA YA LAKI 700 CARWASH YA CCM LEVOLOSI AMKATIA RUFAA HAKIMU ALIYEWAACHIA HURU WASHTAKIWA WA WIZI WALIOONEKANA KWENYE CCTV CAMERA USIKU,ADAI HAKUTENDA HAKI

MLALAMIKAJI KESI YA WIZI WA MAZULIA KUKATA RUFAA

Na Joseph Ngilisho|ARUSHA

ALIYEKUWA Mlalamikaji katika shauri la wizi namba 1101 la mwaka 2026, Nuru Mohamed, Meneja wa Carwash ya CCM Levolosi, amekusudia kukata rufaa baada ya kutoridhishwa na uamuzi wa Mahakama ya Mwanzo Themi wa kuwaachia huru washtakiwa watatu waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma za wizi wa mazulia sita ya wateja.

Mazulia hayo, yenye thamani ya takribani Sh700,000, yalikuwa yamepelekwa katika Carwash hiyo kwa ajili ya kufuliwa kabla ya kudaiwa kupotea katika eneo hilo.

Washtakiwa walioachiwa huru ni Paulo Jeremia, Benjamin Loyishiye na Shaban Kilo.

Kesi hiyo ilisikilizwa na kutolewa uamuzi katika Mahakama ya Mwanzo Themi chini ya Hakimu Mwakila, ambaye katika uamuzi wake aliwaachia huru washtakiwa hao baada ya kubaini kuwa upande wa mlalamikaji haukufanikiwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao kwa kiwango kinachotakiwa kisheria.

Hata hivyo, Mohamed amesema hajaridhishwa na uamuzi huo, akidai kuwa kuna masuala kadhaa katika mwenendo wa kesi na tathmini ya ushahidi ambayo anataka yapitiwe na mahakama ya juu kupitia mchakato wa rufaa.

Miongoni mwa sababu anazozitaja ni madai kwamba alinyimwa haki ya msingi ya kuwauliza washtakiwa maswali wakati wa mchakato wa kesi, jambo analodai lilimnyima fursa ya kutosha ya kuhoji baadhi ya hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi.

Pia, Mohamed anapinga namna ushahidi wa CCTV camera ulivyotathminiwa, akisema kamera hizo zilirekodi matukio yaliyotokea katika eneo la Carwash wakati wa usiku.

Kwa mujibu wa Mohamed, picha za CCTV zilimuonyesha mmoja wa washtakiwa, Paulo Jeremia, akiingia katika eneo hilo na baadaye kuonekana akiondoka akiwa amebeba kapeti.

Mohamed anadai tukio hilo lilitokea wakati shughuli za Carwash zilikuwa zimefungwa na kwamba kapeti hiyo ilikuwa miongoni mwa mazulia yaliyokuwa yamehifadhiwa kwa ajili ya kuoshwa.

Anasema anashangazwa na uamuzi wa mahakama wa kutowatia hatiani washtakiwa hao licha ya ushahidi wa CCTV kuwasilishwa na kupokelewa mahakamani.

“Sijaridhishwa na uamuzi huo. Ninaona kuna ushahidi ambao unahitaji kutazamwa tena, ikiwamo CCTV iliyokuwa ikionyesha matukio yaliyotokea katika eneo la tukio,” amesema Mohamed.

Mohamed amesema hatua yake inayofuata ni kukata rufaa, akitarajia mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza rufaa itapitia upya hoja na ushahidi uliowasilishwa katika shauri hilo.

Kesi hiyo ya wizi namba 1101 ya mwaka 2026 sasa imehitimishwa katika Mahakama ya Mwanzo Themi kwa uamuzi wa Hakimu Mwakila, huku mlalamikaji akisisitiza kuwa anakusudia kutumia haki yake ya kisheria kupinga uamuzi huo kupitia rufaa.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post