Breaking🔥

NAIBU WAZIRI APIGA MARUFUKU MAGARI YA SERIKALI KUBEBA MKAA,AAGIZA YAKAMATWE

 Na Joseph Ngilisho|ARUSHA

NAIBU Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Reuben Kwagilwa, amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri na Majiji kuhakikisha magari ya Serikali yanayobeba mkaa yanakamatwa, akisema Serikali haiwezi kuhimiza upandaji miti wakati taasisi zake zinaendelea kuchangia ukataji wa miti.

Kwagilwa alitoa agizo hilo leo Sep 14,2026 jijini Arusha wakati wa zoezi la upandaji miti katika Shule ya Sekondari Sekei na Shule ya Msingi Kijenge, sehemu ya mpango wa kupanda miti 2,000 katika Jiji la Arusha unaotekelezwa na taasisi ya TEEMO kwa kushirikiana na Benki ya NCBA.

Alisema Serikali imekuwa ikihamasisha wananchi kupanda na kutunza miti ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi, hivyo ni muhimu viongozi wa Serikali kuhakikisha agizo la kuzuia magari ya Serikali kubeba mkaa linatekelezwa.

“Kuanzia leo ni marufuku gari la Serikali kubeba mkaa. Lazima tufanye hivyo ili tuondokane kidogo kidogo na matumizi ya nishati ambayo yanapelekea kukata miti,” alisema.

Alisisitiza kuwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri na Majiji hawapaswi kusubiri maelekezo mengine, bali wanapaswa kusimamia utekelezaji wa agizo hilo na kuhakikisha magari ya Serikali yatakayokiuka yanakamatwa.

“Naagiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri na Majiji kuhakikisha agizo hili linatekelezwa. Gari la Serikali litakalokiuka na kubeba mkaa likamatwe,” alisema.

Kwagilwa alisema Serikali inatambua kuwa jamii bado ina utegemezi mkubwa wa kuni na mkaa kama chanzo cha nishati, lakini akasisitiza kuwa ni lazima mabadiliko ya matumizi ya nishati yafanyike hatua kwa hatua na kuongeza matumizi ya nishati safi na salama.

Alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama, akieleza kuwa juhudi hizo ni muhimu katika kupunguza utegemezi wa nishati inayochangia ukataji wa miti.

Akizungumzia umuhimu wa upandaji miti, Naibu Waziri alisema zoezi hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ambayo inatambua utunzaji wa mazingira na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya maendeleo ya Taifa.

Alisema haitoshi kupanda miti bila kuhakikisha inalindwa na kutunzwa hadi ikue.

“Hatupaswi kupanda miti halafu tunakata miti. Hii haiwezi kuwa na tija. Tunahitaji kuhakikisha miti tunayopanda inatunzwa ili iweze kusaidia kulinda mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema.

Akitoa taarifa katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Benki ya NCBA, Alex Mzirai, alisema benki hiyo imekuwa ikifadhili mpango wa upandaji miti tangu mwaka 2023, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Mzirai alisema kwa mwaka huu benki hiyo inatarajia kufadhili zoezi la upandaji miti 20,000 katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, likihusisha mikoa ya Arusha na Mwanza pamoja na Zanzibar.

Alisema katika mpango huo, Jiji la Arusha limetengewa miti 2,000 ambayo inapandwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Shule ya Sekondari Sekei na Shule ya Msingi Kijenge.

Alisema ushirikiano kati ya sekta binafsi, taasisi zinazoshughulika na mazingira na Serikali ni muhimu katika kuongeza kasi ya uhifadhi wa mazingira, huku akiwataka walengwa wa mradi huo kuhakikisha miti inayopandwa inatunzwa.

Zoezi hilo la upandaji miti 2,000 katika Jiji la Arusha linatekelezwa na TEEMO kwa kushirikiana na Benki ya NCBA, likiwa sehemu ya mpango mpana wa taasisi hiyo wa kuchangia uhifadhi wa mazingira kupitia upandaji miti nchini ili kupunguza majanga mbalimbali kwa binadamu ikiwemo ELNINO.


Ends


Post a Comment

Previous Post Next Post