MNYETI AMNYANG’ANYA MKURUGENZI V8 NA KULIGEUZA AMBULANCE ILI KUBEBEA WAGONJWA NI BAADA YA DED KUSHINDWA KUNUNUA MATAIRI
.... Aagiza hadi ofisi ya Mkurugenzi itakapo nunulia matari Ambulence hiyo ndipo wakomboe V8
Na Joseph Ngilisho|Arushadigital
GEITA. Mkuu wa Mkoa wa Geita, Alexander Mnyeti, amelazimika kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato kutoa gari lake aina ya Land Cruiser V8 na kulitumia kubeba wagonjwa wanaohitaji rufaa katika Kituo cha Afya Muganza, baada ya ofisi yake kushindwa kuhakikisha ambulance ya kituo hicho inapatiwa matairi na kurejesha huduma kwa wananchi.
Agizo hilo limetolewa wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi katika Soko la Kimataifa la Dagaa Kasenda, lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chato, mkoani Geita, ikiwa ni sehemu ya ziara ya Mkuu huyo wa Mkoa ya kujitambulisha kwa wananchi.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mbunge wa Jimbo la Chato Kaskazini, Cornel Magembe, kuwasilisha kero ya kukosekana kwa usafiri wa wagonjwa katika Kituo cha Afya Muganza, akimtaka Mnyeti kuhakikisha ambulance hiyo inapatiwa matairi mapya ili kurejesha huduma ya kuwapeleka wagonjwa wanaohitaji rufaa hospitalini.
Akijibu ombi hilo, Mnyeti ametoa maelekezo ya gari la Mkurugenzi kutumika kama usafiri wa muda wa wagonjwa, huku akisisitiza umuhimu wa hatua za haraka katika kuhakikisha changamoto za huduma za afya haziachi wananchi katika mazingira magumu.
"Dereva wa Mkurugenzi yupo wapi..njoo hapa Leta funguo akazikabidhi kwa dereva wa Ambulance,na kusema kuanzia leo gari hilo litatumika kubebea wagonjwa hadi hapo mtakaponunua matari"Alisisitiza
Agizo hilo limeweka wazi hitaji la uwajibikaji wa viongozi wa halmashauri katika kuhakikisha vifaa na miundombinu ya huduma za msingi, ikiwamo usafiri wa wagonjwa, vinatunzwa na kurekebishwa kwa wakati.
ATOA MAELEKEZO KWA WATUMISHI
Kabla ya kuanza ziara yake ya kujitambulisha kwa wananchi wa Mkoa wa Geita, Mnyeti alitembelea kaburi la aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, lililopo Chato.
Baadaye alikutana na baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato na kuwataka kutekeleza majukumu yao kwa bidii, weledi na uwajibikaji, wakizingatia kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa wakati.
Mnyeti amesema viongozi na watumishi wa Serikali wanapaswa kuelekeza nguvu zao katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na changamoto zao zinatatuliwa kwa ufanisi.
Ends.



Post a Comment