ASKARI 5, MAHABUSU 7 WAFARIKI AJALI YA GARI LA POLISI SEKENKE
By Joseph Ngilisho|ArushaDigital
Ajali hiyo imetokea wakati gari la Polisi likiwa na watu 13, wakiwamo askari watano na mahabusu wanane, waliokuwa wakisafirishwa kutoka Kituo cha Polisi Shelui kwenda Mahakama ya Wilaya ya Iramba iliyopo Kiomboi.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa lori hilo lililokuwa likisafirisha mafuta ya dizeli kutoka Dar es Salaam kuelekea Rwanda, lilipata hitilafu ya breki wakati likishuka katika mteremko wa Mlima Sekenke, kabla ya kuligonga gari hilo la Polisi.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, akisema majeruhi wamepelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Iramba kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, mtu mmoja aliyekuwa katika gari hilo la Polisi amepona ajali hiyo na anaendelea kupatiwa matibabu pamoja na majeruhi wengine.
Ajali hiyo imesababisha mshtuko miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, huku taarifa zaidi kuhusu chanzo cha ajali na utambulisho wa waliopoteza maisha zikitarajiwa kutolewa na mamlaka baada ya uchunguzi kukamilika.
Ends


Post a Comment