VURUGU NAMANGA, POLISI WAPIGA MABOMU YA MACHOZI
...Waandamanaji warusha mawe kituoni, wachoma matairi barabarani huku polisi wakitumia mabomu ya machozi kuwatawanya
...Ni tukio la pili la mauaji ya mawakala wa forodha Namanga, baada ya Steven Kimani kuuawa na mwili wake kukatwa vipande
Kijana Iyan anayedaiwa kuuawa
Na Joseph Ngilisho | LONGIDO
HALI ya taharuki imeendelea kutawala mji wa mpakani wa Namanga, mkoani Arusha, baada ya kundi la vijana, wengi wao raia wa Kenya, kuandamana na kusababisha vurugu mbele ya Kituo cha Polisi Namanga upande wa Tanzania, wakitaka haki itendeke kufuatia mauaji ya kijana mwenzao, Iyan Motema, mwenye umri unaokadiriwa kuwa miaka 24 hadi 25.
Katika kukabiliana na vurugu hizo, polisi wamelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wamekusanyika mbele ya kituo hicho, huku baadhi yao wakidaiwa kurusha mawe na vitu vingine vigumu kuelekea kituoni na kuchoma matairi barabarani.
Vurugu hizo zilianza jana mchana Novemba 3, 2026 na kuendelea hadi leo Novemba 4, huku waandamanaji wakitaka maelezo kuhusu mazingira ya kupotea, kuuawa na kupatikana kwa mwili wa Iyan ndani ya kiroba baada ya kutoweka kwa zaidi ya wiki moja na polisi kuamua kuuzila bila uchunguzi.
Hasira za watu hao zimeelekezwa pia kwa namna tukio hilo lilivyoshughulikiwa, hasa madai kwamba mwili wa marehemu ulizikwa kabla ya kufanyika kwa uchunguzi wa kina na ndugu zake kupata taarifa za uhakika kuhusu hatima yake.
MWILI WAKUTWA NDANI YA KIROBA
Iyan, ambaye alikuwa akijihusisha na shughuli za uwakala wa forodha katika eneo la Namanga, aliripotiwa kutoweka kwa zaidi ya wiki moja, hali iliyosababisha ndugu, marafiki na watu waliokuwa wakimfahamu kuanzisha jitihada za kumtafuta.
Jitihada hizo zilihusisha pia kusambaza taarifa zake kupitia mitandao ya kijamii na makundi mbalimbali ya WhatsApp, lakini hazikufanikiwa kumpata.
Matumaini ya kumpata akiwa hai yalizimika Novemba 3, mwaka huu, baada ya mwili unaodhaniwa kuwa wake kugunduliwa ukiwa ndani ya kiroba kilichotelekezwa eneo la porini.
Kwa mujibu wa maelezo ya watu waliokuwa karibu na eneo hilo, baadhi ya Wamaasai walioliona tukio hilo waliwafahamisha watu wengine, ambao walikusanyika na kwenda kufukua eneo lililokuwa limezikwa kiroba hicho.
Baada ya mwili huo kufukuliwa, ulidaiwa kutambuliwa kuwa wa Iyan, jambo lililochochea hasira miongoni mwa raia wa Kenya wanaoishi na kufanya shughuli zao Namanga.
Wakiwa na hasira, vijana hao walikusanyika na kuelekea kituo cha polisi upande wa Tanzania wakitaka majibu kuhusu mazingira ya tukio hilo, ikiwamo sababu za mwili kuzikwa kabla ya uchunguzi wa kina na taarifa kutolewa kwa ndugu wa marehemu.
Madai kuhusu hatua zilizochukuliwa na polisi katika eneo ulipogunduliwa mwili huo yanahitaji uthibitisho na ufafanuzi wa vyombo husika. Hadi sasa hakuna ushahidi uliowekwa wazi unaothibitisha madai kwamba polisi walihusika na mauaji hayo.
MAUAJI YA PILI YA WAKALA WA FORODHA
Wasiwasi kuhusu usalama wa watu wanaojihusisha na shughuli za uwakala wa forodha Namanga umeongezeka kutokana na tukio jingine la mauaji ya raia wa Kenya, Steven Kimani, ambaye aliuawa kikatili katika makazi yake upande wa Kenya.
Kimani alikutwa ameuawa huku mwili wake ukiwa umekatwa vipande vipande na kuwekwa ndani ya mfuko katika nyumba aliyokuwa akiishi.
Taarifa zilizopatikana zinaeleza kuwa mauaji hayo yaligundulika baada ya mwili kuanza kutoa harufu kali, iliyowafanya majirani kushituka na kufuatilia chanzo chake kabla ya kubaini kuwa kulikuwa na mwili ndani ya nyumba hiyo.
Baada ya kugundua tukio hilo, majirani walitoa taarifa kwa mamlaka husika.
Matukio hayo mawili, yanayohusisha watu waliokuwa wakijihusisha na shughuli za uwakala wa forodha katika mji huo, yameibua maswali kuhusu usalama wa wafanyabiashara na watu wengine wanaotegemea shughuli za mpakani kujipatia kipato.
Pamoja na kufanana kwa mazingira ya vifo hivyo, bado haijathibitishwa kama mauaji ya Iyan na Kimani yana uhusiano wowote au ni matukio mawili tofauti.
Hali hiyo imeongeza umuhimu wa uchunguzi wa kina wa kila tukio ili kubaini wahusika, sababu za mauaji na iwapo kuna mtandao wowote unaohusika na matukio hayo.
Namanga ni kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji kati ya Tanzania na Kenya, kikihudumia wafanyabiashara, wasafirishaji, mawakala wa forodha na wananchi wa mataifa hayo mawili.
Kutokana na umuhimu wake kiuchumi, matukio ya mauaji na vurugu yanaweza kuongeza hofu kwa wafanyabiashara na wananchi wanaotumia mpaka huo kufanya shughuli zao za kila siku.
Hadi habari hii inaandikwa, maswali yaliyokuwa yakisubiriwa majibu ni nani aliyemuua Iyan, kwa nini mwili wake ulikuwa ndani ya kiroba, ulifikaje eneo ulipogunduliwa na ni kwa sababu gani ulidaiwa kuzikwa kabla ya uchunguzi wa kina?
Pia, bado haijafahamika kama kuna uhusiano kati ya mauaji yake na yale ya Steven Kimani, pamoja na hatua zinazochukuliwa kuhakikisha matukio kama hayo hayajirudii.
Jitihada za kumpata Mkuu wa Wilaya ya Longido, Salumu Kalli, na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, ili kupata ufafanuzi kuhusu tukio hilo na hatua za kiusalama zilizochukuliwa, hazikufanikiwa hadi habari hii inaandikwa, baada ya simu zao kutopokelewa.
Mwisho.





Post a Comment