LUGANGIRA AREJESHA MIFUGO 52 ILIYOCHUKULIWA KWENYE MGOGORO WA WAFUGAJI ARUMERU
...Aongoza juhudi za kurejesha amani Kimnyaki na Lengijave, awataka Wamaasai kutotumia nguvu kutatua migogoro
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
MKUU wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Neema Lugangira, amesimamia urejeshaji wa mifugo 52 iliyochukuliwa katika mgogoro uliohusisha jamii mbili za Wamaasai za Kata za Kimnyaki na Lengijave, hatua inayolenga kurejesha amani na utulivu katika maeneo hayo.Mifugo iliyorejeshwa inajumuisha ng’ombe 26, mbuzi 20 na kondoo sita, baada ya Serikali kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na viongozi wa kimila wa jamii ya Wamaasai, maarufu kama Malaigwanani, katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo.
Katika hatua za kushughulikia tukio hilo, Lugangira alifika Kituo cha Polisi Ngaramtoni kupata taarifa za awali kuhusu mgogoro huo na hatua zilizokuwa zimechukuliwa na Jeshi la Polisi kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao.
Baadaye, alikutana na wafugaji wa Kimnyaki na kuwahakikishia kuwa Serikali imeanza kuchukua hatua za kulishughulikia suala hilo, huku akiwataka kutulia na kuepuka vitendo vinavyoweza kuongeza taharuki na kuhatarisha amani.
Lugangira alisema Serikali ina dhamira ya kukutana pia na jamii ya Wamaasai wa Lengijave ili kusikiliza maelezo ya pande zote mbili na kutafuta suluhu ya kudumu kwa njia ya mazungumzo, maridhiano na kwa kuzingatia sheria za nchi.
Alisisitiza kuwa tofauti zinazojitokeza baina ya jamii hazipaswi kuwa chanzo cha wananchi kujichukulia sheria mkononi, akieleza kuwa migogoro inapaswa kutatuliwa kupitia mazungumzo na taratibu zinazotambuliwa kisheria.
Alisema Serikali inatambua na kuheshimu mila na desturi za jamii, lakini hilo halipaswi kutafsiriwa kuwa ruhusa ya kufanya vitendo vinavyokiuka sheria.
Aliongeza kuwa matukio yote yenye viashiria vya uhalifu yanapaswa kuripotiwa katika Jeshi la Polisi ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria badala ya wananchi kuamua kujibu kwa nguvu.
Aidha, aliwataka viongozi wa kimila wa jamii ya Wamaasai (Malaigwanani) kuendelea kushirikiana na Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama katika kuzuia migogoro, kuimarisha maelewano na kuhakikisha amani na mshikamano vinadumu katika jamii hizo.
Ends
Post a Comment