Breaking🔥

KANISA KATOLIKI JIMBO KUU LA ARUSHA KUTABARUKU CATHEDRAL MPYA AGOSTI 7,INAYOGHARIMU SH7.6 BILIONI, BAADA YA MIAKA 15 YA UJENZI

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA


BAADA ya safari ya takriban miaka 15 ya ujenzi, Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha linatarajia kutabaruku Katedrali yake mpya ya Mtakatifu Teresa wa Mtoto Yesu (St. Thérèse) Agosti 7 mwaka huu, ikiwa ni mradi uliogharimu Sh7.6 bilioni na kubeba historia iliyoanza karibu miongo mitatu iliyopita.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 5,2026 jijini Arusha, Mhandisi Mshauri Dkt. Richard John Matolo alisema wazo la kujenga katedrali hiyo liliasisiwa mwaka 1997 na aliyekuwa Askofu wa Pili wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Hayati Fortunatus Lukanima, kabla ya kumaliza kipindi chake cha uaskofu mwaka 1998.

Alisema baada ya Askofu Lukanima kustaafu, mrithi wake, Askofu Josephat Louis Lebulu, aliendeleza maono hayo kupitia mchakato mpana uliowashirikisha viongozi wa Kanisa, mapadri, walei na wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi, hatua iliyowezesha kufikiwa uamuzi wa kujenga katedrali hiyo katika eneo la Sanawari, jijini Arusha.

Dkt. Matolo alisema ujenzi ulianza rasmi mwaka 2011 na hadi sasa umechukua takriban miaka 15, huku gharama zake zikifikia Sh7.6 bilioni, kiwango kilicho karibu na makisio ya awali ya Sh7 bilioni yaliyowekwa wakati mradi huo ulipoanza.

"Ni jambo la kushukuru kwamba licha ya kupita kwa muda mrefu wa ujenzi, gharama halisi zimebaki karibu na makadirio ya awali. Hii ni mafanikio makubwa kwa mradi wa aina hii," alisema.

Alieleza kuwa katedrali hiyo imejengwa kwa kuzingatia viwango vya makanisa makuu ya kikatoliki duniani, ikiwemo kuwa na minara miwili yenye urefu wa mita 50 kila mmoja, kiwango kinachozidi urefu wa kawaida wa mita 45 unaopatikana katika katedrali nyingi.

Mbali na hilo, alisema jengo hilo lina eneo maalumu la kuhifadhi makaburi ya maaskofu (Crypt) lenye nafasi tisa, ambalo litatumika kuhifadhi masalia ya maaskofu waliolitumikia Jimbo Kuu la Arusha baada ya kuhamishwa kutoka maeneo walikozikwa sasa.

"Kathedrali ndiyo kanisa lenye hadhi ya juu zaidi ndani ya jimbo. Hapa ndipo makao makuu ya Askofu wa Jimbo, na ndiyo kitovu cha shughuli zote muhimu za Kanisa Katoliki katika Jimbo Kuu la Arusha," alisema.

Kwa mujibu wa Dkt. Matolo, katedrali hiyo itakapokamilika kikamilifu itaweza kupokea waumini wapatao 3,500 kwa wakati mmoja wakiwa wamekaa.

Akizungumzia upekee wa jengo hilo, alisema mbali na usanifu wake wa kisasa, lina sifa adimu duniani kwa kuwa limejengwa katikati ya mikondo miwili ya maji inayolizunguka eneo la Sanawari.

Alisema kwa mtazamo wa kiimani, maji hayo yanaashiria neema, uzima na uwepo wa Mungu, akirejea maandiko matakatifu ya Ezekieli 47, Zaburi 46 na Ufunuo 22 yanayozungumzia maji kama ishara ya baraka na uhai wa kiroho.

Kuhusu ibada ya kutabaruku, Dkt. Matolo alisema ratiba kamili pamoja na orodha ya wageni watakaohudhuria itatangazwa na Kamati ya Maandalizi ya Kutabaruku Katedrali, huku akitoa mwaliko kwa waumini na wananchi wote kushiriki tukio hilo ambalo linaandika ukurasa mpya katika historia ya Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha.






ENDS

Post a Comment

Previous Post Next Post