MWANAMKE AUAWA KWA MAZINGIRA YA KUTISHA, MUME AMZIKA NDANI YA NYUMBA KILOSA; POLISI WAMSAKA MTUHUMIWA

 MWANAMKE AUAWA KWA MAZINGIRA YA KUTATISHA, AZIKWA NDANI YA NYUMBA KILOSA; POLISI WAMSAKA MTUHUMIWA

Na Arushadigital | MOROGORO

Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linaendesha msako mkali wa kumtafuta mwanaume mmoja anayedaiwa kuhusika na mauaji ya mwanamke aliyefahamika kwa jina la Lilian Daniel (27), mkulima na mkazi wa Kijiji cha Changalawa, Wilaya ya Kilosa, ambaye inadaiwa aliuawa na mwanaume aliyekuwa akiishi naye kama mume na mke kisha mwili wake kufukiwa ndani ya nyumba waliyokuwa wanaishi.

Kwa mujibu wa taarifa za awali kutoka Jeshi la Polisi, tukio hilo lilifichuka Machi 8, 2026, baada ya ndugu na baadhi ya wananchi kuanza harakati za kumtafuta Lilian aliyekuwa hajulikani alipo tangu Desemba 2025.

Inaelezwa kuwa baada ya jitihada za muda mrefu za kumtafuta bila mafanikio, ndugu wa marehemu waliinua shaka juu ya mwanaume aliyedaiwa kuwa na uhusiano wa karibu naye. Hivyo waliamua kufika katika nyumba aliyokuwa akiishi mwanaume huyo wakiamini huenda angekuwa na taarifa muhimu kuhusu mahali alipo Lilian.

Walipofika katika nyumba hiyo na kufanya uchunguzi wa awali, waligundua uwepo wa sehemu iliyofukiwa ndani ya nyumba ambayo ilionekana kuwa na dalili za kaburi. Hali hiyo iliwatia wasiwasi na kuwalazimu kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili kuchunguza zaidi.

Baada ya polisi kufika eneo la tukio na kufanya uchunguzi wa kina, walifanikiwa kuufukua mwili uliokuwa umefukiwa ndani ya nyumba hiyo, ambao ulithibitishwa kuwa wa mwanamke aliyekuwa akitafutwa.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini chanzo halisi na mazingira ya mauaji hayo, huku juhudi kubwa zikiendelea kumtafuta mtuhumiwa mkuu wa tukio hilo.

Aidha, Polisi wametoa wito kwa wananchi wenye taarifa zozote zinazoweza kusaidia kupatikana kwa mtuhumiwa huyo, ambaye jina lake bado halijawekwa wazi, kujitokeza na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola kwa kufika katika kituo chochote cha Polisi kilicho karibu au kuwataarifu viongozi wa Serikali za mitaa.

Mamlaka hizo pia zimehimiza wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu kwa wakati ili kusaidia kudhibiti vitendo vya kikatili vinavyoathiri usalama wa jamii.


Ends. 

Post a Comment

0 Comments