MVUA KUBWA ZASITISHA USAFIRI ARUSHA–LOLIONDO, MAFURIKO YATATIZA BARABARA, LOLIONDO COACH YABWAGA MANYANGA HOFU KUPANDA KWA BIDHAA NGORONGORO

 MVUA KUBWA ZASITISHA USAFIRI ARUSHA–LOLIONDO, MAFURIKO YATATIZA BARABARA

Na Joseph Ngilisho | NGORONGORO

 

SHUGHULI za usafirishaji wa abiria na mizigo kati ya Arusha na Loliondo zimesimama kwa muda kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika Mkoa wa Arusha, hali iliyosababisha mafuriko makubwa katika baadhi ya mito na kufanya barabara hiyo kushindwa kupitika kwa usalama.


Mvua hizo zinazoendelea kunyesha katika ukanda wa Bonde la Ufa hususan maeneo ya Lake Natron pamoja na maeneo ya hifadhi za Serengeti na Ngorongoro, zimesababisha makampuni ya usafirishaji kusitisha safari hadi hapo hali ya hewa itakapotengamaa.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa Kampuni ya Usafirishaji wa Abiria ya Loliondo Coach, John Kimambo, amesema uamuzi huo umechukuliwa kwa lengo la kulinda usalama wa abiria na magari kutokana na mafuriko makubwa yaliyosababisha barabara kutopitika.


Amesema kwa zaidi ya siku saba sasa mito ya Monick iliyopo katika Kijiji cha Engaresero na Athuman iliyopo katika Kijiji cha Engaruka imefurika na kusababisha changamoto kubwa kwa vyombo vya usafiri vinavyopita katika eneo hilo.


Kwa mujibu wa Kimambo, hali hiyo imekuwa ikiwasababishia madereva na abiria kusubiri kwa muda mrefu mbungani ili maji yapungue kabla ya kuvuka mito hiyo, lakini katika siku za hivi karibuni kiwango cha maji kimeongezeka zaidi na kufanya hali kuwa hatari.


“Hali ya hewa kwa sasa ni mbaya sana. Kwa siku ya saba mfululizo mito ya Monick na Athuman imejaa mafuriko makubwa. Siku tatu zilizopita tulikuwa tunasubiri hata kwa saa kumi maji yapungue ndipo magari yapite, lakini tangu jana maji yameongezeka zaidi,” amesema Kimambo.


Ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo, kampuni imelazimika kurudisha mabasi yaliyokuwa yakitoka Arusha hadi Mto wa Mbu ili abiria wapate huduma mbadala, huku mabasi yaliyokuwa yakitokea Loliondo yakisimamishwa katika eneo la Engaruka hadi hali ya hewa itakaporuhusu safari kuendelea.


Kimambo amesema hatua hiyo imechukuliwa ili kuepusha ajali au uharibifu wa magari ambao unaweza kuhatarisha maisha ya abiria.


Mbali na kusitisha huduma kwa muda, pia ametoa wito kwa Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuchukua hatua za haraka kuboresha barabara ya Arusha–Loliondo ili kuondoa changamoto zinazojirudia kila msimu wa mvua.


Amesema uzoefu wa zaidi ya miaka 20 wa kampuni hiyo katika kutoa huduma za usafiri katika barabara hiyo unaonesha kuwa suluhisho la kudumu ni kujengwa kwa barabara ya lami pamoja na madaraja imara katika mito inayokatiza barabara hiyo.


“Tunaiomba Serikali iangalie barabara hii kwa jicho la tofauti. Tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan aielekeze Serikali kuboresha miundombinu ya barabara hii, kwa sababu inasumbua sana wakati wa mvua na hata kiangazi magari yanaharibika kutokana na ubovu wa barabara,” alisisitiza Kimambo.


Barabara ya Arusha–Loliondo ni moja ya njia muhimu inayotumiwa na wakazi wa Wilaya ya Ngorongoro pamoja na watalii wanaotembelea maeneo ya Lake Natron na hifadhi jirani, hivyo kusitishwa kwa usafiri katika kipindi hiki kunatarajiwa kuathiri shughuli za kiuchumi na kijamii katika ukanda huo.


Ends...

Post a Comment

0 Comments