UBALOZI WA MAREKANI WASHAMBULIWA KWA RISASI

 UBALOZI WA MAREKANI TORONTO WASHAMBULIWA KWA RISASI

Na Joseph Ngilisho | Arushadigital

WATU wasiojulikana wameripotiwa kushambulia Ubalozi wa Marekani uliopo jijini Toronto nchini Canada kwa kutumia silaha za moto, katika tukio ambalo mamlaka za usalama zimelielezea kuwa linahusishwa na masuala ya usalama wa taifa.

Kwa mujibu wa taarifa za awali kutoka kwa vyombo vya usalama, shambulio hilo lilitokea mapema Jumanne asubuhi ambapo watu hao walifyatua risasi kadhaa kuelekea kwenye jengo la ubalozi huo kabla ya kutoweka kusikojulikana.

Maafisa wa polisi waliowasili katika eneo la tukio walifanikiwa kukusanya maganda ya risasi yaliyokuwa yametapakaa karibu na jengo hilo, huku uchunguzi wa kina ukiendelea ili kubaini wahusika pamoja na chanzo halisi cha tukio hilo.

Ingawa hakuna taarifa zilizotolewa mara moja kuhusu watu kujeruhiwa au kupoteza maisha, mamlaka zimeeleza kuwa shambulio hilo linachukuliwa kwa uzito mkubwa kutokana na kulenga moja kwa moja jengo la kidiplomasia.

Kwa upande wake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imethibitisha kufahamu tukio hilo na kueleza kuwa inaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya uchunguzi kwa kushirikiana na vyombo vya sheria vya Canada.

“Tunafahamu tukio lililotokea katika Ubalozi wetu wa Toronto na tunaendelea kushirikiana na mamlaka za usalama za Canada kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanyika,” ilieleza sehemu ya taarifa ya wizara hiyo.

Tukio hilo linakuja siku chache baada ya polisi nchini Norway kuanza uchunguzi kufuatia mlipuko uliotokea nje ya Ubalozi wa Marekani uliopo jijini Oslo siku ya Jumapili, hali inayoongeza tahadhari ya kiusalama katika balozi za Marekani katika baadhi ya mataifa ya Ulaya na Amerika Kaskazini.

Mamlaka za usalama zimeongeza ulinzi katika maeneo muhimu ya kidiplomasia huku uchunguzi ukiendelea ili kubaini iwapo matukio hayo mawili yana uhusiano wowote.

Uchunguzi zaidi unaendelea, huku polisi wakiwahimiza wananchi wenye taarifa zozote zinazoweza kusaidia kufanikisha uchunguzi huo kujitokeza na kushirikiana na vyombo vya dola.


Ends..

Post a Comment

0 Comments