TRAFIKI ADAKWA AKIOMBA RUSHWA YA ELFU 10 KWA KIINGEREZA KIBOVU KWA RAIA WA KIGENI

 By Arushadigital -Arushadigital

Jeshi la Polisi mkoani Iringa linamshikilia askari wa usalama barabarani kwa tuhuma za kuomba  rushwa ya sh,elfu 10 , baada ya kuonekana katika picha mjongeo (video) inayosambaa mitandaoni akidaiwa kupokea fedha kutoka kwa dereva wa gari la watalii alilokuwa amelisimamisha barabarani.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, askari huyo alisimamisha gari hilo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni ukaguzi wa kawaida wa barabarani. Hata hivyo, katika video hiyo, askari huyo anaonekana akiwasiliana na dereva kwa muda kabla ya kudaiwa kupokea fedha kwa njia isiyo rasmi, tukio lililozua mjadala mpana miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa alisema jeshi hilo limechukua hatua za haraka mara baada ya video hiyo kuibuka, na kwamba askari anayehusishwa na tukio hilo tayari amekamatwa kwa ajili ya uchunguzi wa kina.

“Jeshi la Polisi halitavumilia vitendo vya rushwa wala ukiukwaji wa maadili ya kazi. Uchunguzi unaendelea, na hatua kali za kisheria zitachukuliwa endapo tuhuma zitathibitika,” alisema Kamanda huyo.

Aidha, Jeshi la Polisi limewataka wananchi na wageni wanaotumia barabara nchini kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa au ukiukwaji wa sheria, huku likisisitiza kuwa linajitahidi kuimarisha uwajibikaji na uadilifu kwa askari wake.

Tukio hilo limeibua upya mjadala kuhusu nidhamu na maadili ya askari wa usalama barabarani, hasa katika maeneo yanayotumiwa na watalii, ambapo serikali imekuwa ikisisitiza umuhimu wa kulinda taswira ya nchi na kukuza sekta ya utalii.

Post a Comment

0 Comments