MWIGULU ATAHADHALISHA HALI YA UKAME NCHINI,ATAKA WAKULIMA KUTUNZA VYAKULA

 Na ArushaDigital – Dodoma

Waziri Mkuu atoa tahadhari ya ukame, wananchi watakiwa kutumia akiba ya chakula kwa uangalifu


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba, ametoa tahadhari kuhusu hali ya ukame inayolikabili taifa kufuatia kuchelewa kwa msimu wa mvua, huku akiwataka Watanzania kutunza na kutumia kwa uangalifu akiba ya chakula waliyonayo.


Wito huo umetolewa Desemba 14, mwaka huu, wakati Waziri Mkuu alipokutana na baadhi ya Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kutoka mikoa ya Dodoma na Singida katika ofisi zake Mlimwa, jijini Dodoma.


Akizungumza katika kikao hicho, Dk. Mwigulu alisema Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa utabiri wa mwelekeo wa mvua za vuli na mvua za msimu kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025, pamoja na mvua za msimu wa Novemba 2025 hadi Aprili 2026. Kwa mujibu wa utabiri huo, baadhi ya maeneo nchini yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani, hali itakayochangia vipindi virefu vya ukame na mtawanyiko usioridhisha wa mvua.


“Kwa kuzingatia utabiri huo, baadhi ya mikoa nchini inatarajiwa kukumbwa na mvua chache, hali itakayodumisha vipindi virefu vya ukavu,” alisema Waziri Mkuu.


Alifafanua kuwa tathmini ya TMA inaonesha uwezekano wa kuchelewa kwa msimu wa mvua katika mikoa ya Dodoma, Katavi, Kigoma, Singida, Tabora, Iringa, Mbeya, Mtwara, Njombe, Songwe, Rukwa, Ruvuma pamoja na maeneo ya kusini mwa Mkoa wa Morogoro.


Hata hivyo, Dk. Mwigulu alihakikishia wananchi kuwa kwa sasa hakuna tishio la uhaba wa chakula nchini, akibainisha kuwa taifa lina hifadhi ya chakula ya kutosha. Pamoja na hilo, aliwasihi wananchi kuendelea kuwa waangalifu katika matumizi ya chakula na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima.


“Ingawa tuna akiba ya chakula ya kutosha, ni muhimu wananchi wakaendelea kuweka akiba na kutumia chakula kwa nidhamu,” alisisitiza.


Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwakumbusha wakulima kuandaa mashamba yao kwa wakati na kutumia pembejeo zinazofaa kulingana na upatikanaji wa mvua chache. Pia aliwahimiza kuzingatia ushauri wa wataalamu wa kilimo ambao kwa sasa wanaendelea kutoa elimu kwa wakulima katika maeneo mbalimbali nchini.


Kwa upande wa wafugaji, Dk. Mwigulu aliwataka kuweka mipango madhubuti ya matumizi na uhifadhi wa maji pamoja na chakula cha mifugo ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na hali ya ukame.


Vilevile, aliwasisitiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuhakikisha maafisa ugani wanawatembelea wakulima mara kwa mara mashambani na kuwapatia ushauri wa kitaalamu, ikiwemo matumizi sahihi ya mbegu kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa, badala ya kukaa ofisini kwa muda mrefu.


“Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri endeleeni kuhamasisha wakulima wajisajili kwenye daftari la mkulima na kuhakikisha wanapata namba za usajili,” alisema.


Aidha, aliizitaka taasisi za umma ikiwemo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) kuhakikisha shehena za pembejeo zinahudumiwa kwa wakati bandarini ili kurahisisha usambazaji wake kwa wakulima nchini kote.


Hatua hizo, kwa mujibu wa Waziri Mkuu, ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa chakula unaendelea kudumishwa licha ya changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa.

Post a Comment

0 Comments