Breaking🔥

WAKULIMA 37 WAREJESHEWA SH MILIONI 100 ZA RIBA BAADA YA KUREJESHA MKOPO KWA WAKATI

 WAKULIMA 37 WAREJESHEWA SH MILIONI 100 ZA RIBA

Na Joseph Ngilisho | Arusha


WAKULIMA 37 kutoka maeneo mbalimbali nchini wamepokea takribani Sh milioni 100, ikiwa ni sehemu ya asilimia 50 ya riba waliyolipa baada ya kurejesha kwa wakati mikopo waliyopewa kwa ajili ya ununuzi wa mashine na vifaa vya kilimo.

Fedha hizo zimetolewa kupitia Interest Rebate Programme ya kampuni ya Equity for Tanzania Limited (EFTA), mpango unaolenga kuwahamasisha wakulima kuwa na nidhamu ya kifedha na marejesho ya mikopo.


Katika mpango huo, jumla ya Sh milioni 43 zilirejeshwa mwaka 2025 kwa wakulima 15, huku mwaka huu wakulima wengine 22 wakirejeshewa Sh milioni 53, na kufanya jumla ya fedha zilizorejeshwa kufikia takribani Sh milioni 100 kwa wanufaika 37.

Hafla ya kuwatambua wanufaika hao na kukabidhiwa hundi za mfano ilifanyika katika banda la EFTA kwenye Maonesho ya Nanenane 2026 jijini Arusha, mbele ya wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo.

Mmoja wa wanufaika, Erimiti Mushi kutoka Arusha, alisema upatikanaji wa mashine kupitia ufadhili wa EFTA umebadili kwa kiasi kikubwa namna anavyotekeleza shughuli zake za kilimo.

Alisema awali alitumia zana za kawaida ambazo zilichukua muda mrefu katika utekelezaji wa shughuli za kilimo na kuongeza gharama za uzalishaji

“Baada ya kupata mashine, nimeweza kuongeza eneo la kilimo, kuongeza uzalishaji na pia kutoa huduma kwa wakulima wengine katika eneo langu,” alisema.

Kwa upande wake, Sebastian Gwaltu kutoka Katesh, Manyara, alisema mashine alizopata zimemsaidia kupunguza changamoto katika maandalizi ya mashamba, uvunaji na uchakataji wa mazao.

Alisema kurejeshewa sehemu ya riba aliyolipa ni motisha kwa wakulima kuendelea kuwa na nidhamu katika marejesho ya mimikopo.

Mbali na manufaa kwa wakulima hao, uwekezaji huo umechangia pia kuibua fursa za ajira kwa zaidi ya watu 300 wanaohusika katika shughuli mbalimbali za kilimo.

Walionufaika na fursa hizo ni pamoja na madereva wa matrekta, waendesha mashine, mafundi pamoja na vibarua wanaoshiriki katika uzalishaji na uchakataji wa mazao.

Kwa kutumia mashine, wakulima hao wameweza kuhudumia mashamba makubwa zaidi kwa muda mfupi, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ufanisi wa shughuli za kilimo.

Hatua hiyo imechangia kuongezeka kwa kipato cha wakulima na familia zao, huku pia ikipanua fursa za kiuchumi kwa watu wanaowazunguka.

EFTA imesema nidhamu ya marejesho iliyoonyeshwa na wakulima imekuwa na manufaa si kwa wanufaika pekee, bali pia kwa taasisi hiyo ya kifedha.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, kiwango cha mikopo chechefu (Non-Performing Loans – NPL) kilifikia asilimia moja Juni mwaka huu, kiwango ambacho kimeelezwa kuwa miongoni mwa viwango vya chini kwa taasisi za fedha nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa EFTA, Nicomed Bohay, alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya kampuni hiyo na wateja wake.

“Interest Rebate Programme ni zaidi ya kurejesha sehemu ya riba kwa wateja wetu. Tunataka kujenga utamaduni wa nidhamu ya kifedha unaowanufaisha wakulima na wakati huo huo kuifanya taasisi yetu iendelee kuwa imara ili iweze kuwafikia wakulima wengi zaidi,” alisema.

Bohay alisema nidhamu ya marejesho ya wakulima hao imechangia kwa kiasi kikubwa kufikiwa kwa kiwango cha asilimia moja cha mikopo chechefu, hali inayoiwezesha EFTA kuendelea kutoa ufadhili kwa wakulima na wajasiriamali wengine nchini.

Kadiri mahitaji ya chakula na mazao ya biashara yanavyoongezeka, uwekezaji katika mashine na vifaa vya kisasa unatajwa kuwa miongoni mwa njia muhimu za kuongeza tija na ushindani wa kilimo nchini.

Kupitia ufadhili wa mali, wakulima wanaweza kupata matrekta, power tillers, mashine za uchakataji wa mazao na vifaa vingine vya kilimo ambavyo kwa kawaida vinaweza kuwa vigumu kununuliwa kwa fedha taslimu.

Kwa wakulima 37 walionufaika na mpango wa Interest Rebate, uzoefu wao unaonyesha kuwa kupata mashine ni hatua ya kwanza, lakini matumizi sahihi ya mashine pamoja na nidhamu ya marejesho ya mkopo ndiyo msingi wa kuvuna manufaa zaidi.

Rejesho la takribani Sh milioni 100 walilopokea ni sehemu ya matokeo ya nidhamu hiyo, huku likitoa ujumbe kwamba uaminifu katika marejesho unaweza kuwa kichocheo cha wakulima wengi zaidi kupata fursa ya ufadhili wa mashine na vifaa vya kisasa.

MWISHO



Post a Comment

أحدث أقدم