NAIBU WAZIRI AINGIA KATI MGOGORO WA ARDHI MONDULI, SIMANJIRO
.....Aagiza chanzo cha mgogoro wa miaka 15 kichambuliwe, wananchi wadai kurejeshewa zaidi ya hekta 2,600
Na Joseph Ngilisho | Monduli
NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya, ameingia kati mgogoro wa ardhi wa takribani miaka 15 kati ya wananchi wa Kijiji cha Oldonyo, Kata ya Lemoot, Wilaya ya Monduli na wenzao wa Kijiji cha Lobusoit A, Wilaya ya Simanjiro, na mwekezaji wa Shamba Namba 24 la Maasai Stepple Conservancy Ltd.
Mmuya amesema lengo la Serikali ni kujenga uelewa wa pamoja kuhusu chanzo cha mgogoro huo ili kuwezesha pande zote kujenga hoja ya kupata suluhisho, ikiwemo madai ya wananchi kuhusu maeneo wanayodai kupoteza kutokana na uwekezaji huo.
Akizungumza leo, Agosti 7, 2026, katika Ofisi ya Kijiji cha Oldonyo, wakati wa mkutano na wananchi wa maeneo hayo, Mmuya alisema Serikali inalenga kuchambua umiliki wa eneo hilo na namna ambavyo mwekezaji alipata ardhi hiyo.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa katika mkutano huo, mwekezaji anamiliki kihalali jumla ya hekta 3,425, huku wananchi wa Monduli wakidai ziada ya hekta 870.3 na wananchi wa Simanjiro wakidai hekta 1,778.3.
Madai hayo yakijumuishwa yanafikia hekta 2,648.6, ambayo wananchi wanataka suala lake liangaliwe katika mchakato wa kutafuta suluhisho la mgogoro huo.
Mmuya alisema hatua ya kwanza ni kubaini historia ya eneo hilo, ikiwemo lini, nani na kwa utaratibu gani mwekezaji alipewa ardhi hiyo inayogusa maeneo ya Halmashauri za Wilaya za Monduli na Simanjiro.
“Tunataka kuelewa chanzo cha mgogoro huu, lini na namna gani mwekezaji alipewa jumla ya hekta 3,425 na namna eneo hilo lilivyohusisha pande mbili za Monduli na Simanjiro,” alisema Mmuya.
Alisema uelewa huo utasaidia Serikali, wananchi na mwekezaji kuwa na msingi mmoja wa majadiliano katika kutafuta suluhisho la mgogoro huo ambao umedumu tangu mwaka 2011.
MBUNGE: MONDULI NA SIMANJIRO ZINAHITAJI ARDHI
Mbunge wa Monduli, Isack Joseph Copriano, amesema wananchi wa Monduli na Simanjiro wanahitaji ardhi kwa ajili ya shughuli zao za kiuchumi na kijamii, hivyo anaamini Serikali itapata suluhisho litakalorejesha matumaini kwa wananchi.
“Monduli tunahitaji ardhi na Simanjiro wanahitaji ardhi; sote tunahitaji ardhi irudi mikononi mwetu. Kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan alisema anapoondoka madarakani hataki kuwaachia Watanzania matatizo bali amani, ninaamini tutapata majibu mazuri yenye kurejesha furaha kwa wananchi wa Monduli na Simanjiro,” alisema.
Copriano alisema anaamini hatua iliyochukuliwa na Naibu Waziri inaweza kuwa mwanzo wa kumaliza mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu.
WANANCHI: ARDHI NI MUHIMU KWA MALISHO
Mwenyekiti wa Kijiji cha Oldonyo, Saitoti Mwatuni, amemuomba Naibu Waziri kuupa kipaumbele mgogoro huo ili upatiwe suluhisho la haraka.
Mwatuni alisema eneo linalogombaniwa ni muhimu kwa wananchi wa kijiji hicho kwa kuwa wanategemea ardhi hiyo kwa shughuli za ufugaji, hususan malisho ya mifugo.
Alisema kuchelewa kwa suluhisho kunaendelea kuwaweka wananchi katika hali ya sintofahamu kuhusu matumizi ya ardhi wanayoitegemea kwa maisha yao.
MWENYEKITI: NI MWANZO WA MIGOGORO MINGINE
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Kisioki Moitiko, amesema wananchi wamefurahishwa na hatua ya Naibu Waziri kufika katika eneo hilo kama alivyoahidi wakati wa ziara ya Waziri Mkuu katika Viwanja vya Barafu, Mto wa Mbu, Monduli.
Moitiko alisema ujio huo ni ishara nzuri kwamba Serikali imeanza kuchukua hatua za kutafuta mwafaka wa mgogoro huo.
“Ni furaha kwa wananchi kuona kwamba ahadi aliyoitoa Mhe. Kaspar Mmuya wakati wa ujio wa Waziri Mkuu katika Viwanja vya Barafu, Mto wa Mbu, leo ametimiza. Tunaona huu ni mwanzo mzuri wa kufikia mwafaka wa mgogoro huu,” alisema.
Aidha, Moitiko alisema anaamini hatua hiyo inaweza kuwa mwanzo wa kutatuliwa kwa migogoro mingine ya ardhi katika Halmashauri ya Monduli, ikiwemo inayodaiwa kuwepo Mfereji, Selela na maeneo mengine.
MMUYA: TUTAKAA NA MWEKEZAJI
Akihitimisha ziara hiyo, Mmuya alisema Serikali haitaliacha suala hilo bila kulifanyia kazi, akiahidi kushirikiana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Leonard Akwilapo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo pamoja na Mbunge wa Monduli, Copriano, katika mchakato wa kutafuta suluhisho.
Alisema hatua inayofuata ni kukaa pamoja na mwekezaji wa Shamba Namba 24 ili kujadili kwa kina historia ya umiliki wa eneo hilo, madai ya wananchi na namna ya kupata mwafaka unaoweza kumaliza mgogoro huo.
Mgogoro huo umeendelea kwa takribani miaka 15 tangu mwaka 2011, huku wananchi wa pande zote mbili wakidai kuwa eneo hilo ni muhimu kwa shughuli zao za maisha, ikiwemo ufugaji na malisho ya mifugo.
Ends






إرسال تعليق