GARI LA WATALII LATUMBUKIA KWENYE KORONGO SERENGETI, WATU WANNE WANUSURIKA KIFO
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
HIFADHI YA TAIFA SERENGETI imeingia kwenye tahadhari baada ya gari la utalii lenye namba za usajili T 377 BJE kutumbukia mtoni katika eneo la Kogatende, Kivuko cha Nyumbu Namba Moja, ndani ya hifadhi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) leo Agosti 31, 2026, imeeleza kuwa ajali hiyo ilitokea majira ya saa 8:00 mchana, wakati gari hilo likiwa katika shughuli za utalii.
Kwa mujibu wa TANAPA, gari hilo lilikuwa mali ya Kampuni ya Utalii ya Nature Responsible Safari Company Limited, na lilikuwa likiendeshwa na Ramadhani Miraji Mbaga (Mtanzania).
Katika ajali hiyo, dereva pamoja na watalii wanne, raia wa Uswisi, walifanikiwa kunusurika baada ya gari hilo kutumbukia mtoni.
HATUA ZA HARAKA ZACHUKULIWA
TANAPA imesema hatua za awali za kukabiliana na tukio hilo tayari zimechukuliwa, huku uchunguzi wa kina ukiendelea ili kubaini chanzo cha ajali hiyo na mazingira yaliyopelekea gari hilo kutoka kwenye eneo la njia na kutumbukia mtoni.
Taarifa hiyo, iliyosainiwa na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Catherine Mbena, imeeleza kuwa mamlaka itaendelea kufuatilia tukio hilo kwa karibu.
TANAPA pia imetoa wito kwa madereva, wageni pamoja na kampuni zote za utalii zinazofanya shughuli ndani ya hifadhi kuzingatia kwa umakini sheria na taratibu za matumizi ya vivuko, hususan katika maeneo ambayo yanahusisha kuvuka mito na maeneo yenye changamoto za kijiografia.
TANAPA YATOA ONYO KALI
Shirika hilo limeonya kuwa uzembe au ukiukwaji wa taratibu za uhifadhi na usalama katika maeneo ya vivuko unaweza kusababisha madhara makubwa kwa wageni, mali na wanyamapori.
“Uzembe au ukiukwaji wa taratibu unaweza kusababisha madhara makubwa yanayoweza kuepukika kwa kufuata taratibu za Hifadhi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Tukio hilo linaongeza umuhimu wa kuimarishwa kwa tahadhari na uzingatiaji wa taratibu za usalama katika maeneo ya vivuko ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, ambayo hupokea maelfu ya watalii kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kushuhudia wanyamapori na ikolojia yake.
TANAPA imesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea, huku taarifa zaidi zikitarajiwa kutolewa baada ya kukamilika kwa uchunguzi.
Picha kwa hisani ya Mtandao
Ends

إرسال تعليق