DC MKUDE AZITAKA NGOs KUACHA UBAGUZI, ZISHIRIKIANE NA SERIKALI
.......NACONGO yalalamikia kupungua kwa ufadhili, yaomba ubia mpya wa Serikali na sekta binafsi
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MKUU wa Wilaya ya Arusha, Joseph Modestin Mkude, amezitaka taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) kuacha kufanya kazi kwa kujitenga na Serikali, akiwataka kujenga ushirikiano wa karibu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Mkude alisema hayo wakati akifungua Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Arusha, lililowakutanisha viongozi wa Serikali, mashirika ya kiraia na wadau wa maendeleo kujadili nafasi ya NGOs katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Alisema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na mashirika hayo katika sekta mbalimbali, ikiwemo afya, elimu, maji, uwezeshaji wa kiuchumi, mazingira na kusaidia makundi yenye mahitaji maalumu.
Kwa mujibu wa Mkude, Mkoa wa Arusha una mashirika 1,206 yaliyosajiliwa, lakini si yote yana uwezo wa kutekeleza miradi kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo ufinyu wa rasilimali.
Aliwataka NGOs kuhakikisha miradi yao inaendana na mahitaji halisi ya wananchi, inatekelezwa kwa uwazi na inazingatia sheria, taratibu na ushirikishwaji wa wadau.
“Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na mashirika haya, ni lazima yaendelee kuzingatia sheria na taratibu katika utekelezaji wa shughuli zao,” alisema.
Mkude alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa mashirika hayo na kutoa ushirikiano pale yanapohitaji msaada, akisisitiza kuwa Serikali na asasi za kiraia zina wajibu wa pamoja katika kuchochea maendeleo.
Aidha, Mkude aliyataka mashirika hayo kutumia fursa zinazotokana na kuaminiwa kwa Arusha kuwa mwenyeji wa matukio makubwa ya kitaifa na kimataifa.
Alitaja miongoni mwa matukio hayo kuwa ni Mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) unaotarajiwa kufanyika Arusha, akisema NGOs zinapaswa kutumia majukwaa hayo kuelimisha wananchi na kuonyesha mchango wao katika maendeleo.
“Kikubwa zaidi ni umoja wenu, kwa sababu mkishirikiana mnaweza kuchangia kufanikisha mambo makubwa,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Nguvila, alisema NGOs ni wadau muhimu katika mchakato wa maendeleo kwa sababu shughuli zao zinagusa moja kwa moja maisha ya wananchi.
Alisema baadhi ya mashirika yamekuwa yakifanya kazi katika kuwawezesha wananchi kiuchumi, ikiwemo kuwasaidia kupata mikopo kupitia benki na taasisi za fedha.
Alitaja pia afya, elimu, maji, michezo, uwezeshaji wa kiuchumi na kusaidia familia na makundi maalumu kuwa miongoni mwa maeneo ambayo NGOs zimekuwa zikitoa mchango.
“Mashirika yote ambayo yamejikita katika kusaidia ustawi wa jamii na maendeleo katika nyanja mbalimbali ni wadau muhimu katika mwelekeo wa maendeleo,” alisema Dkt. Nguvila.
Alisema ushirikiano kati ya Serikali na NGOs ni muhimu katika kuhakikisha rasilimali zinazopatikana kutoka kwa wadau mbalimbali zinatumika kwa ufanisi na kuleta matokeo yanayokusudiwa.
NACONGO YALIA UFADHILI
Wakati Serikali ikisisitiza ushirikiano, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACONGO) alisema kupungua kwa ufadhili ni miongoni mwa changamoto kubwa inayozikabili NGOs nchini.
Alisema mabadiliko ya vipaumbele vya wafadhili na kupungua kwa fedha kumeathiri uwezo wa baadhi ya mashirika kutekeleza programu zao, hali inayolazimisha sekta hiyo kutafuta mbinu mpya za kupata rasilimali.
“Changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni rasilimali za kuendesha mashirika yetu na kazi tunazozifanya, hususan baada ya ufadhili kupungua au kutokuwepo, au wafadhili kubadilisha maeneo wanayoyapa kipaumbele,” alisema.
Alisema NGOs zinapaswa kuacha kutegemea chanzo kimoja cha fedha na badala yake kubuni vyanzo vipya vya rasilimali, ikiwemo kujenga ubia na Serikali, sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo.
“Tunataka kuwa na fikra mpya, kuangalia zaidi ubia na namna ya kupata rasilimali kupitia vyanzo mbalimbali,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema NACONGO itaendelea kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu katika kuboresha mazingira ya utendaji wa NGOs na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya taifa.
Mjadala huo umeibua umuhimu wa kujenga mfumo mpya wa ushirikiano kati ya Serikali, NGOs, sekta binafsi na wadau wa maendeleo, hasa katika kipindi ambacho upatikanaji wa fedha za wafadhili unaendelea kuwa changamoto kwa mashirika mengi.
NACONGO imewataka wadau wa sekta hiyo kutumia majukwaa ya kitaifa kujadili changamoto zao na kuweka mikakati mipya ya kuhakikisha NGOs zinaendelea kuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa ajenda za maendeleo.
Mwenyekiti huyo pia alitoa mwito kwa NGOs kushiriki kikamilifu katika Jukwaa la Kitaifa linalotarajiwa kufanyika Dodoma, akisema litatoa nafasi ya kujadili mustakabali wa sekta hiyo na kutafuta majibu ya changamoto zinazoikabili.
Ends

إرسال تعليق