DC KARANGA ATAKA WAZAZI WASIWANYIME WATOTO FURSA YA ELIMU,AMZAWADIWA MWANAFUNZI MIL1.
......Asema kutolipa ada, kutowafuatilia na kutowapeleka shule kunawanyima nafasi za ajira; Bayo asema Tumaini sasa kuwekeza zaidi kwenye michezo
Na Joseph Ngilisho | KARATU
MKUU wa Wilaya ya Karatu, Lameck Karanga, amewataka wazazi kutokwepa wajibu wa kuwasomesha watoto wao, akisema kutowapeleka shule, kutolipa ada kwa wakati na kutofuatilia maendeleo yao ni miongoni mwa sababu zinazoweza kuwanyima fursa za ajira na maisha bora baadaye.
Karanga alitoa kauli hiyo leo Agosri 29,2026 akiwa mgeni rasmi katika mahafali ya Shule za Tumaini Junior na Tumaini TX wilayani Karatu, ambako alisisitiza kuwa jukumu la kumjenga mtoto haliwezi kuachwa kwa shule pekee.Alisema wazazi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika elimu ya watoto wao kwa kuhakikisha wanahudhuria masomo, ada zinalipwa kwa wakati na maendeleo yao yanafuatiliwa mara kwa mara.
“Usipompeleka mtoto shule, usipolipa ada kwa wakati na usipomtembelea mtoto, unamnyima mtoto fursa ya kupata ajira katika nyanja mbalimbali,” alisema Karanga.
Aliwataka wazazi kutambua vipaji vya watoto wao mapema na kuviunga mkono, akisema elimu ya darasani na vipaji vinapaswa kwenda sambamba katika kumuandaa mtoto kukabiliana na maisha ya baadaye.
Karanga pia aliipongeza sekta binafsi kwa mchango wake katika kutoa elimu, akisema Serikali haiwezi kufanya kila kitu peke yake katika kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bora.
Alimpongeza Mkurugenzi wa Shule za Tumaini Junior na Tumaini TX, Bodest Bayo, pamoja na walimu na timu nzima ya shule hizo kwa uwekezaji wao katika elimu na malezi ya watoto.
Alisema ushirikiano kati ya Serikali, shule binafsi, wazazi na wadau wengine wa elimu ni muhimu katika kujenga kizazi chenye maarifa, nidhamu na uwezo wa kuliletea taifa maendeleo.
Karanga pia alifurahishwa na vipaji vilivyooneshwa na wanafunzi katika mahafali hayo,alimpongeza mwanafunzi,Viola Tibikunda kwa kuonesha kipaji chakuelezea utendaji kazi mzuri wa serikali kwa kumzawadia kiasi cha sh,milioni 1 fedha tasilimu, akisisitiza kuwa elimu haipaswi kuishia darasani.Alisema michezo, sanaa, sayansi, teknolojia na shughuli nyingine za ubunifu ni sehemu ya kuwaandaa watoto kwa fursa zinazopatikana katika dunia ya sasa.
BAYO: TUMAINI KUWAANDAA VIJANA KWA ELIMU NA MAADILI
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shule za Tumaini Junior na Tumaini TX, Bodest Bayo, alisema taasisi hiyo haijikita katika ufaulu wa mitihani pekee, bali inalenga kuwajenga wanafunzi kielimu, kimaadili, kinidhamu na kimichezo.Bayo alisema wanafunzi wa Darasa la Saba waliohitimu wamepitia safari ya elimu iliyoanzia madarasa ya awali hadi kumaliza elimu ya msingi, hivyo hatua hiyo haipaswi kutafsiriwa kuwa mwisho wa safari yao.
“Huu si mwisho wa safari, bali ni mwanzo wa hatua nyingine ya elimu ya sekondari na baadaye chuo kikuu. Tunawategemea mfanye vizuri zaidi katika hatua zinazofuata,” alisema.
Aliwataka wahitimu kutumia kipindi cha mapumziko kwa nidhamu, kuwasaidia wazazi katika shughuli za nyumbani na kuendelea kujisomea badala ya kujiingiza katika makundi na tabia zisizofaa.
Bayo alisema shule hizo pia zimekuwa zikisisitiza uzalendo, maadili na historia ya Tanzania ili kuwajenga wanafunzi kuwa raia wema na viongozi wa baadaye.
Katika hatua nyingine, Bayo alisema Tumaini imeamua kuongeza nguvu katika michezo kupitia Tumaini Schools Sport Academy, programu inayolenga kuibua na kukuza vipaji vya wanafunzi tangu wakiwa shuleni.Alisema programu hiyo imerasimishwa na kusajiliwa katika Baraza la Michezo la Taifa, hatua itakayowezesha shule kuendelea kuwafuatilia wanafunzi wenye vipaji hata baada ya kumaliza masomo.
“Tunataka mwanafunzi akitoka shule hapa tuendelee kumfuatilia na kumjengea uwezo hadi aweze kufikia timu kubwa. Lengo ni kuhakikisha michezo inakuwa fursa kwa wanafunzi wetu,” alisema.
Bayo alitoa mfano wa aliyekuwa mwanafunzi wa shule hizo, Saint Toti Kashiro, akisema alitumia kipaji chake cha mpira wa kikapu kushiriki mashindano ya Afrika Mashariki na Kati na baadaye kupata ajira katika Jeshi la Magereza kutokana na uwezo wake katika michezo.
Alisema mfano huo unaonesha kuwa kipaji cha mtoto kikipewa mazingira sahihi kinaweza kuwa daraja la kupata ajira na kujenga maisha.
TUMAINI YAJIANDAA KWA AFCON 2027
Bayo alisema Tumaini Senior Secondary School iliyopo Makuruni, Monduli, imeanza kuimarisha zaidi programu za michezo kwa kuajiri makocha na kuandaa timu zitakazoshiriki mashindano mbalimbali.
Alisema maandalizi hayo pia yanaangalia fursa zitakazotokana na Tanzania kuwa mwenyeji mwenza wa AFCON 2027, akisema vijana wanapaswa kuandaliwa mapema ili kunufaika na fursa zinazoweza kujitokeza kupitia michezo.
TUMAINI TX YASISITIZA TAALUMA, MALEZI
Alisema wanafunzi hushiriki katika michezo, kilimo, uimbaji, skauti, midahalo na shughuli nyingine zinazolenga kuwajenga kwa mtazamo mpana zaidi ya masomo ya darasani.
Kimatia alisema shule pia imeanzisha Hope Studio kwa ajili ya kukuza vipaji vya uimbaji na Tumaini School Sports Academy kwa ajili ya michezo.
TAALUMA YANG’ARA
Kwa mujibu wa Kimatia, katika matokeo ya mwaka wa masomo 2025, wanafunzi wa Darasa la Saba walipata wastani wa daraja A, huku Darasa la Nne likipata daraja B, mafanikio yaliyoiwezesha shule hiyo kuingia katika shule 10 bora kwa ngazi ya Wilaya ya Karatu.
Alisema hayo yalikuwa matokeo ya kwanza ya shule hiyo kufanya mtihani wa Darasa la Saba.
Kimatia alisema mwaka huu wanafunzi saba wamehitimu Darasa la Saba, wakiwamo wavulana wanne na wasichana watatu.
Alisema katika mahafali ya mwaka uliopita, wanafunzi 14 walihitimu, ambapo 13 walipata wastani wa daraja A na mmoja daraja B.
MICHEZO, KILIMO KUJENGA UJUZI
Kimatia alisema shule imeendelea kuimarisha michezo, huku wanafunzi wake wawili, Alfred na Riwards, wakishiriki mpira wa kikapu kupitia UMITASHUMTA hadi ngazi ya mkoa.
Pia alisema shule imeanzisha bustani za mboga, matunda na miti ya vivuli, zinazowapa wanafunzi nafasi ya kujifunza kilimo na utunzaji wa mazingira.
Alisema baadhi ya mazao yanayozalishwa hutumika katika upatikanaji wa mboga kwa ajili ya chakula cha wanafunzi.
CHANGAMOTO NI MIUNDOMBINU
Pamoja na mafanikio hayo, Kimatia alisema shule bado inahitaji ushirikiano wa wadau katika kuboresha miundombinu, ikiwamo ujenzi wa madarasa ya awali, ofisi za walimu na taaluma pamoja na chumba cha ushauri na unasihi.
Alisema shule pia inahitaji maktaba yenye vitabu, bwalo la chakula na kompyuta mpakato kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Mahafali hayo yalikuwa sehemu ya jitihada za shule za Tumaini kuendeleza mkazo katika elimu, malezi, maadili, michezo na vipaji, huku viongozi wakisisitiza ushirikiano wa wazazi, walimu, Serikali na sekta binafsi katika kumwandaa mtoto kwa maisha na ajira za baadaye.
Ends















Post a Comment