TANAPA YANYAKUA TUZO 6, SERENGETI, KILIMANJARO, TARANGIRE ZATINGA KILELENI
Na Joseph Ngilisho | ZANZIBAR
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeendeleza ubabe wake katika sekta ya utalii duniani baada ya kunyakua tuzo sita za kimataifa za World Travel Awards (WTA) 2026, katika hafla iliyofanyika usiku wa Agosti 28, 2026, Zanzibar.
Tuzo hizo, zilizotolewa katika hafla ya Africa Gala Ceremony iliyofanyika katika Hoteli ya Diamond Bijoux, Bwejuu, Zanzibar, zimeongeza heshima kwa Tanzania katika soko la utalii duniani, huku Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ikiongoza kwa kutwaa tuzo mbili.
Serengeti ilitwaa tuzo mbili za Africa’s Leading National Park 2026 na Africa’s Leading Big Five National Park 2026.
Hifadhi nyingine zilizotwaa tuzo ni Tarangire, iliyotambuliwa kama Africa’s Leading Elephant Paradise National Park 2026; Nyerere, iliyotwaa Africa’s Leading Scenic National Park 2026; Ruaha, iliyotambuliwa kama Africa’s Leading Cultural National Park 2026; na Kilimanjaro, iliyotwaa tuzo ya Africa’s Leading Mountain National Park 2026.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwanzilishi na Rais wa World Travel Awards, Graham Cooke, alisema ni heshima kubwa kwa taasisi hiyo kuifanya Zanzibar kuwa mwenyeji wa hafla hiyo mwaka huu.
Cooke alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazokua kwa kasi katika sekta ya utalii, huku akieleza kuwa ongezeko la watalii katika fukwe za Zanzibar na hifadhi za taifa linaendelea kutoa mchango katika uchumi wa nchi.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazokua kwa kasi sana katika sekta ya utalii na inaendelea kuweka rekodi ya watalii wengi katika maeneo ya fukwe za Zanzibar na katika Hifadhi za Taifa,” alisema.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo, Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Massana Mwishawa, alisema ushindi huo unaonyesha nafasi muhimu ya Tanzania katika uhifadhi wa maliasili na kukuza utalii endelevu.
Mwishawa alisema tuzo hizo ni sehemu ya utambuzi wa kimataifa wa juhudi zinazofanywa na Tanzania katika kulinda rasilimali za Taifa ambazo ni msingi wa sekta ya utalii.
Alisema ongezeko la watalii na uwekezaji katika maeneo ya hifadhi lina mchango katika kuongeza mapato yanayowezesha Serikali kuboresha huduma na miundombinu katika maeneo mbalimbali.
“Kupitia tuzo hizo, Hifadhi za Taifa Tanzania zimeendelea kuvutia watalii wengi na wawekezaji ambao huchagiza ongezeko la mapato yanayotumika katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali, zikiwemo barabara, huduma za maji safi na salama na afya,” alisema.
Mwishawa pia alihusisha mafanikio hayo na jitihada za Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha sekta ya utalii na kuongeza utangazaji wa vivutio vya Tanzania katika masoko ya kimataifa.
Alitaja matumizi ya filamu za “Tanzania – The Royal Tour” na “Amazing Tanzania”, pamoja na sera za Diplomasia ya Uchumi, kuwa miongoni mwa hatua zilizosaidia kuongeza mwonekano wa Tanzania katika ramani ya utalii duniani.
Kwa upande wa TANAPA, ushindi wa tuzo hizo sita unatoa fursa zaidi ya kuitangaza Tanzania katika masoko ya ndani na kimataifa, huku ukilenga kuongeza idadi ya watalii na kuimarisha uelewa kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa rasilimali za Taifa.
Ushindi huo pia unaongeza hadhi ya hifadhi za Tanzania katika ushindani wa kimataifa, hasa katika kipindi ambacho nchi inaendelea kuweka mikakati ya kukuza utalii na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.
World Travel Awards ni miongoni mwa tuzo zinazotambua ubora katika sekta ya usafiri na utalii duniani. Washindi hupatikana kupitia mchakato wa upigaji kura unaoshirikisha wadau na washiriki wa sekta hiyo katika ngazi mbalimbali.
Ends ...





Post a Comment