AJALI YA BAJAJI NA LORI YAUWA WAWILI PAPO HAPO MURIET-ARUSHA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
WATU wawili wamefariki dunia papo hapo katika ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha bajaji na lori la kubeba mchanga katika eneo la Dampo, Mtaa wa Murieti, Kata ya Sokoni One, jijini Arusha.
Ajali hiyo imetokea baada ya bajaji iliyokuwa ikitokea eneo la Intel kuelekea katikati ya Jiji la Arusha kugongana na lori lililokuwa likisafirisha mchanga kwa ajili ya ujenzi wa barabara.
Kwa mujibu wa taarifa za awali kutoka eneo la tukio, bajaji hiyo ilikuwa imebeba abiria wanne pamoja na dereva wakati ilipohusika katika ajali hiyo.
Katika ajali hiyo, abiria wawili walifariki dunia papo hapo baada ya kupata majeraha makubwa, huku taarifa zaidi kuhusu hali ya abiria wengine zikisubiriwa kutoka kwa mamlaka husika.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa dereva wa lori aliondoka eneo la tukio mara baada ya ajali hiyo, kabla ya baadaye kujisalimisha katika Kituo cha Polisi Murieti, jijini Arusha.
Jeshi la Polisi lilifika katika eneo la tukio na kuchukua miili ya marehemu na kuipeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya taratibu zaidi.
Aidha, magari yaliyohusika katika ajali hiyo yaliondolewa eneo la tukio ili kurejesha hali ya kawaida ya usafiri na kupunguza msongamano uliotokana na ajali hiyo.
Hadi sasa, majina ya watu waliofariki hayajatangazwa rasmi, huku chanzo cha ajali hiyo kikisubiriwa kuthibitishwa na Jeshi la Polisi.
Taarifa zaidi zinatarajiwa kutolewa na mamlaka husika kuhusu chanzo cha ajali, idadi na hali ya majeruhi pamoja na utambulisho rasmi wa marehemu.
Ends


Post a Comment