KOPLO MWITA AFARIKI MAHABUSU YA POLISI TANGA
Na Joseph Ngilisho | TANGA
ASKARI wa Jeshi la Polisi namba H.1796, Koplo Mwita, amefariki dunia akiwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Wilaya ya Tanga, ambako alikuwa akishikiliwa kwa ajili ya uchunguzi wa tuhuma za kijinai.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga, Koplo Mwita alikutwa amefariki dunia ndani ya chumba cha mahabusu Agosti 27, 2026, majira ya saa 1:03 usiku.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa kabla ya kifo chake, marehemu alikuwa miongoni mwa askari sita wa Jeshi la Polisi waliokuwa wakishikiliwa kwa tuhuma za kijinai, akiwamo afisa mmoja na askari wengine watano wa vyeo mbalimbali.
Baada ya tukio hilo, uchunguzi wa kisayansi ulifanyika huku ndugu wa marehemu wakishuhudia, ambapo kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi huo, chanzo cha kifo kilibainika kuwa ni kukosa hewa kutokana na kujinyonga.
Jeshi hilo limeeleza kuwa mwili wa marehemu tayari umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya taratibu za mazishi, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
POLISI YAWAONYA WANANCHI
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limewaonya baadhi ya wananchi, vyombo vya habari na watumiaji wa mitandao ya kijamii dhidi ya kuandaa au kusambaza taarifa zisizothibitishwa kuhusu tukio hilo.
Polisi imesema ni muhimu kwa taarifa zinazohusu tukio hilo kuzingatia matokeo rasmi ya uchunguzi, ikisisitiza kuwa kutoa hitimisho lisilotokana na uchunguzi rasmi kunaweza kusababisha upotoshaji na kuwa kinyume cha sheria.
Jeshi hilo limeongeza kuwa uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea kukamilishwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zote za kiuchunguzi.
Aidha, Polisi Mkoa wa Tanga imesisitiza kuwa hatua zote zinazohusu tukio hilo zitafanyika kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa kisheria ili kubaini kwa ukamilifu mazingira ya kifo cha Koplo Mwita.
Ends



Post a Comment