TANAPA YATOA AGIZO ZITO KWA KITENGO CHA MAHUSIANO YA JAMII

TANAPA YATOA AGIZO ZITO KWA KITENGO CHA MAHUSIANO YA JAMII

Na Joseph Ngilisho | DODOMA

KAMISHNA wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massana Mwishawa, amekitaka Kitengo cha Mahusiano ya Jamii kuongeza wigo wa utoaji wa elimu ya uhifadhi kwa wananchi, hususan jamii zinazoishi kuzunguka hifadhi za taifa, ili kuongeza ushiriki wao katika kulinda na kuhifadhi maliasili.

Mwishawa amesisitiza kuwa elimu ya uhifadhi ni nyenzo muhimu katika kujenga uelewa kwa wananchi na kuimarisha mahusiano kati ya TANAPA na jamii zinazozunguka hifadhi, akieleza kuwa jamii zinapaswa kuwa sehemu muhimu ya juhudi za uhifadhi.

Akizungumza katika Kikao Kazi cha Mwaka cha Kitengo cha Mahusiano ya Jamii, kinachofanyika jijini Dodoma, Kamishna huyo alisema elimu hiyo inapaswa kuwafikia wananchi kwa upana na kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazohusiana na uhifadhi na wanyamapori.

Alisema maeneo muhimu yanayopaswa kupewa kipaumbele ni pamoja na elimu ya namna ya kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu, athari za mabadiliko ya tabianchi, umuhimu wa uhifadhi wa vyanzo vya maji pamoja na fursa za uzalishaji mali zinazotokana na sekta ya utalii.

Aidha, alikitaka kitengo hicho kuimarisha elimu kuhusu usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya ujirani mwema, inayolenga kuimarisha mahusiano na ushirikiano kati ya hifadhi na jamii zinazozunguka maeneo hayo.

Mwishawa alisema ushirikishwaji wa jamii katika uhifadhi haupaswi kuishia katika utoaji wa taarifa pekee, bali wananchi wanapaswa kuelewa umuhimu wa maliasili na kuona namna wanavyoweza kunufaika na fursa zinazotokana na uhifadhi na utalii.

Alisema TANAPA inalenga kujenga jamii yenye uelewa mpana wa masuala ya uhifadhi na utayari wa kushiriki kikamilifu katika kulinda maliasili, hatua ambayo itasaidia kupunguza migogoro kati ya wananchi na wanyamapori na kuimarisha uhifadhi shirikishi.

Kwa mujibu wa Kamishna huyo, ushirikiano wa karibu kati ya TANAPA na jamii zinazozunguka hifadhi ni msingi muhimu wa kuhakikisha maliasili zinalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Alisisitiza kuwa kuimarishwa kwa elimu na ushirikishwaji wa wananchi kutasaidia kujenga mazingira ya kuaminiana, kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za uhifadhi na hatimaye kuhakikisha uhifadhi endelevu wa maliasili nchini.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم