Breaking🔥

BOT YASEMA: UHARIBIFU WA FEDHA NI HASARA KWA TAIFA CHUMA ULETE WACHANGIA ,YASHINDA TUZO SEKTA YA FEDHA NANE NANE ARUSHA


 Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema uharibifu wa fedha unaofanywa na baadhi ya wananchi, ukiwamo kukata noti kwa sababu za imani za kishirikina, unasababisha hasara kwa taifa kwa kuwa fedha hizo hulazimika kuondolewa kwenye mzunguko na kutengenezwa upya.

BoT imesema fedha hizo zingetumika katika shughuli nyingine za maendeleo, ikiwamo kuboresha huduma za afya, kununua dawa, kujenga barabara na kugharamia shughuli nyingine za kijamii zenye manufaa kwa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa  na Cretus Joseph Mwakalinga, Meneja wa Operesheni wa BoT Kanda ya Arusha, wakati akizungumza katika maonyesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Arusha.

Mwakalinga alisema ingawa si kila fedha inayoharibiwa inaweza kutafsiriwa moja kwa moja kuwa hasara kwa kiwango sawa, uharibifu wake kwa ujumla una athari kwa uchumi kutokana na gharama na rasilimali zinazotumika kuiondoa kwenye mzunguko.

“Fedha hii ingeweza kufanya kazi nyingine. Tungeweza kwenda hospitalini, kununua dawa, kuwalipa vizuri madaktari, kujenga barabara au kufanya shughuli nyingine za kijamii ambazo zingeweza kunufaisha zaidi jamii kuliko kuiharibu,” alisema.

Alisema noti inapokatwa, kuchanwa au kuharibiwa kwa namna nyingine na hatimaye kufika BoT, huondolewa kwenye mzunguko kwa sababu wananchi wana haki ya kutumia fedha zilizo katika hali nzuri.

Akizungumzia sababu zinazowafanya baadhi ya wananchi kuharibu noti, Mwakaringa alisema bado kuna imani za kishirikina zinazowafanya baadhi yao kukata pembe za fedha wakiamini kuwa hatua hiyo itawalinda dhidi ya kile kinachoitwa chumaulete.

“Unakuta mwananchi kwa ajili ya imani hizo anachukua fedha yetu, anaikata kwenye pembe akiamini kwamba akikata kule, chumaulete haitaweza kuchukuliwa. Tunachosema ni kwamba huo ni uharibifu wa fedha,” alisema.

Alisema tabia hiyo huondoa ubora wa noti na hatimaye fedha hiyo inapofika BoT hulazimika kuondolewa kwenye mzunguko.

Mwakaringa aliwataka wananchi kutumia fedha kwa namna inayokusudiwa na kuacha imani zinazowafanya kuzikata au kuziharibu.

BoT pia imewataka wananchi kuacha hofu na imani zinazowafanya kuhifadhi sarafu bila kuzitumia katika miamala ya kawaida.

Mwakaringa alisema kulikuwa na kipindi ambacho baadhi ya watu waliamini kuwa kumpa mtu mwingine sarafu zao kungeweza kusababisha fedha zao kupotea.

“Ilifika mahali unakuta mtu ana ndoo nzima ya sarafu lakini hawezi kumpa jirani yake chenji, akiamini kwamba akitoa zile sarafu na kumpa mwingine, fedha zake zitaondoka,” alisema.

Alisema sarafu zipo za kutosha na wananchi wanapaswa kuzitumia katika miamala yao badala ya kuzihifadhi kwa sababu za imani.

Katika hatua nyingine, BoT imesema bado kuna changamoto kubwa kwa baadhi ya wakulima katika matumizi na utunzaji wa fedha, huku ikiwataka kutumia mifumo rasmi ya kifedha.

Mwakaringa alisema baadhi ya wakulima bado wana mtazamo wa zamani wa kuficha fedha majumbani baada ya kuuza mazao yao, jambo linaloweza kuwaweka katika hatari ya kupoteza fedha hizo.

Alisema BoT imekuwa ikihimiza malipo ya wakulima yapitie benki ili kuwawezesha kutunza fedha zao kwa usalama na kupanga matumizi.

Hata hivyo, alisema changamoto hujitokeza pale mkulima anapopokea malipo na kutoa fedha zote kwa wakati mmoja.

“Fedha ikifika benki na mkulima akaambiwa malipo yake yamefika, anaenda kuchukua fedha yote. Sasa akichukua hela yote, anaenda kuiweka sehemu nyingine ambazo siyo salama,” alisema.

Alisema BoT imeendelea kutoa elimu ya fedha katika kata na maeneo mbalimbali, ikiwamo maonyesho ya Nanenane, ili kuwasaidia wakulima na wananchi kwa ujumla kujenga utamaduni wa kutunza fedha, kupanga matumizi na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

Mwakaringa alisema maandalizi ya mapema ndiyo siri ya BoT kuendelea kufanya vizuri katika maonyesho ya Nanenane na kupata tuzo mbalimbali.

Alisema benki hiyo huweka pamoja wataalamu kutoka sekta tofauti ili kuhakikisha wananchi wanaopata fursa ya kutembelea banda lake wanapata majibu na elimu kuhusu masuala ya fedha.

“Siri yetu kubwa ni maandalizi. Tunajiandaa. Tuna madawati tofauti, kuna dawati la uchumi, taasisi za fedha, masuala ya benki, sarafu na pia dawati la malalamiko,” alisema.

Alisema mfumo huo unawezesha BoT kuwafikia wananchi, hasa wakulima, na kuwapatia elimu kulingana na mahitaji yao.

“Tunapokuja kwenye maonyesho ya Nanenane, tunataka kumfikia mkulima kwa kila ambacho atakuwa na hitaji la elimu. Tunafanya maandalizi ya kutosha na kila sekta inakuwepo hapa,” alisema.


Ends...

Post a Comment

أحدث أقدم