NANENANE YAFUNGUA NJIA YA MASOKO, MAKALLA AWATAKA WAZALISHAJI KUONGEZA TIJA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MAONYESHO ya Nanenane⁰ Kanda ya Kaskazini yamevunja rekodi mwaka huu, huku Serikali ikiwataka wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali kubadili mtazamo wa uzalishaji kwa kuanza na mahitaji ya soko badala ya kuzalisha bila kuwa na uhakika wa wanunuzi.
Hatua hiyo inalenga kuwawezesha wazalishaji kutumia fursa za masoko zitakazotokana na Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ambayo Tanzania itakuwa mwenyeji mwenza.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, alisema hayo Agosti 8,2026 jijini Arusha wakati akimwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais–TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, katika kilele cha Maonyesho ya 32 ya Nanenane yaliyofanyika katika Viwanja vya Njiro.
Makalla, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya maonyesho hayo, alisema ongezeko la ubora wa mabanda, ushiriki wa wadau pamoja na matumizi ya teknolojia katika kilimo, mifugo na uvuvi, vimeifanya Nanenane ya mwaka huu kuwa ya kipekee.
“Kwa kweli maonyesho ya safari hii yamevunja rekodi. Mabanda yetu ni mazuri na yana vitu vingi vya kujifunza,” alisema.
Makalla alisema kaulimbiu ya mwaka huu, “Tambua Soko, Ongeza Tija kwa Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” inapaswa kutafsiriwa kwa vitendo na kuwa msingi wa uzalishaji katika sekta zote za kilimo, mifugo, uvuvi na ujasiriamali.
Alisema kuongeza uzalishaji bila kuzingatia mahitaji ya soko kunaweza kumweka mzalishaji katika hasara, akisisitiza umuhimu wa kujua bidhaa inayohitajika, ubora unaotakiwa na soko linalolengwa kabla ya kuanza uzalishaji.
“Safari ya uzalishaji inaanzia sokoni. Mkulima, mfugaji na mvuvi wa leo anatakiwa kuzalisha kwa kuzingatia mahitaji ya soko, ubora unaohitajika na viwango vinavyokubalika ndani na nje ya nchi,” alisema.
Kwa mujibu wa Makalla, Tanzania inapaswa kuachana na uzalishaji wa mazoea na kuelekea katika uzalishaji unaozingatia ubora, tija na ushindani ili bidhaa za ndani ziweze kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Makalla alisema maandalizi ya AFCON 2027 yanapaswa kutazamwa kama fursa ya kiuchumi kwa wazalishaji wa ndani, badala ya kuangaliwa kama mashindano ya michezo pekee.
Alisema wafanyabiashara na wazalishaji wanapaswa kuanza maandalizi mapema kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vinavyoweza kukidhi mahitaji ya wageni na masoko yatakayofunguka wakati wa mashindano hayo.
“Wakati wa mwezi wa nane AFCON inaanza. Ninaamini kabisa tukiwa na maonyesho yenye bidhaa nzuri na zenye ubora, tunaweza kwenda kupata masoko ndani na nje ya nchi,” alisema.
Alisema Arusha na Kanda ya Kaskazini zina nafasi kubwa ya kunufaika kutokana na uwepo wa masoko ya nchi jirani, miundombinu ya usafirishaji, ardhi, maji, mifugo pamoja na taasisi za utafiti na mafunzo.
Makalla alitaja shughuli za biashara katika maeneo ya mipakani, hususan Namanga, kuwa mfano wa ukubwa wa soko linaloweza kunufaisha wakulima na wafugaji.
“Ukienda Namanga unaona malori mengi yanayobeba mahindi kutoka katika mikoa yetu. Hii ni fursa kwa wakulima kuona soko na bei nzuri yenye faida,” alisema.
Katika hotuba hiyo, Serikali ilisisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na mifugo, ikisema uchakataji umeanza kuwafungulia wajasiriamali masoko mapya na kuongeza kipato.
Ilisema bidhaa nyingi zinazopatikana katika maduka makubwa zimeanzia kwenye mazao yanayozalishwa nchini, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuwekeza zaidi katika uchakataji.
“Leo ukienda kwenye supermarket kubwa, unaona wajasiriamali wetu wamepata nafasi ya kusambaza bidhaa mbalimbali. Mambo mengi yameanza kutokana na mazao yetu. Hii inatia moyo kuona kwamba uchakataji na uongezaji thamani umechukua nafasi,” ilisema Serikali.
Serikali ilisema mafanikio hayo yanahitaji kuimarishwa kwa uwekezaji katika uhifadhi, usafirishaji, bima ya kilimo na huduma za kifedha, ili kuwawezesha wazalishaji kukabiliana na changamoto za uzalishaji na masoko.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alisema Nanenane inapaswa kuwa chachu ya kubadili maisha ya wakulima na wafugaji kwa kuwapatia maarifa, teknolojia na mbinu bora wanazoweza kuzitumia wanaporejea katika maeneo yao.
Babu alisema maonyesho hayo yanatoa nafasi kwa wakulima kutoka mikoa mbalimbali kujifunza na kubadilishana uzoefu, hivyo ziara za mabanda hazipaswi kuwa shughuli ya kutazama bidhaa pekee.
“Wakulima na wafugaji wanapopata fursa hii ya Nanenane, jambo kubwa ni kuja kujifunza na kubadilishana uzoefu,” alisema.
Babu alisisitiza matumizi ya mbolea na pembejeo bora, kisema hali ya udongo katika maeneo mbalimbali nchini inahitaji wakulima kutumia mbolea ili kuongeza uzalishaji.
“Bila kutumia mbolea hatuwezi kupiga hatua. Lazima tutumie mbolea kutokana na ardhi yetu ilivyo sasa,” alisema.
Alisema Tanzania pia ina mbegu bora zinazofanyiwa majaribio, akibainisha kuwa endapo zitathibitishwa na wataalamu kuwa na uwezo mkubwa wa kuongeza mavuno, zinaweza kuwa miongoni mwa teknolojia zitakazobadili uzalishaji wa mazao nchini.
Babu alisema Tanzania imejaliwa ardhi nzuri na rasilimali nyingi za kilimo, hivyo kinachohitajika ni kuzitumia kwa ufanisi zaidi kwa kuunganisha maarifa, teknolojia na pembejeo.
“Tumebarikiwa sana kuwa na ardhi nzuri Tanzania. Kubwa ni kuitumia vizuri ili tupate manufaa makubwa,” alisema.
Ends...



إرسال تعليق