Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dk Johannes Lembulung Lukumay, aliwataka wakulima kuchangamkia fursa za kilimo, akisema Serikali imewekeza zaidi ya Sh20 bilioni katika ruzuku ya mbegu na mbolea kwa wakulima wa jimbo hilo.
Lukumay alisema uwekezaji huo unaonyesha dhamira ya Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuifanya sekta ya kilimo kuwa kichocheo cha uchumi wa wananchi, huku akiwataka wakulima kutumia fursa hiyo kuongeza uzalishaji na kipato.
Alisema kati ya fedha hizo, zaidi ya Sh17 bilioni zilitolewa kwa ajili ya ruzuku ya mbegu, huku takribani Sh3 bilioni zikitumika katika ruzuku ya mbolea.
Lukumay alisema hayo Agosti 8,2026 katika kilele Cha Maadhimisho ya sikukuu ya wakulima Nane Nane Njiro, jijini Arusha,alipokuwa akizungumza na wakulima, wajasiriamali na wananchi baada ya kutembelea banda la Halmashauri ya Arusha muda mfupi baada ya kutua nchini akitokea London Nchini Uingereza.
“Nimshukuru sana Mheshimiwa Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika kilimo na kwa upendo wake kwa wananchi. Katika Jimbo la Arumeru Magharibi ameweza kuwekeza zaidi ya Sh17 bilioni kwenye ruzuku ya mbegu na Sh3 bilioni kwenye ruzuku ya mbolea,” alisema.
Kwa mujibu wa Lukumay, uwekezaji huo umepunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima na kuwawezesha kutumia pembejeo bora, jambo alilosema linaweza kuongeza tija na ubora wa mazao.
Alisema fursa hiyo inapaswa kwenda sambamba na matumizi sahihi ya mbegu na mbolea pamoja na kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo ili wakulima wanufaike kikamilifu na uwekezaji huo.
AWATAKA WANANCHI KUTUMIA MIKOPO
Mbunge huyo pia aliwataka wananchi, hususan wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kuchangamkia mikopo inayotolewa na halmashauri na kuitumia kama mtaji wa kuongeza shughuli za uzalishaji.
Alisema katika ziara yake alikutana na vikundi vya wanawake vilivyonufaika na mikopo hiyo na kuanzisha miradi mbalimbali, ikiwamo kilimo, ufugaji wa nyuki na uzalishaji wa asali.
“Waende sasa, wajisajili kwenye vijiji vyao, wakachukue mikopo halmashauri. Hii inaweza kumsaidia mtu mmoja mmoja kuongeza kipato chake na kuinua uchumi,” alisema.
Lukumay alisema Halmashauri ya Wilaya ya Arusha imefanya vizuri katika utekelezaji wa mpango huo baada ya kusajili vikundi 202, ikilinganishwa na lengo la vikundi 150.
Alisema mafanikio hayo yanaonyesha mwitikio wa wananchi katika kutumia fursa za Serikali kujenga mitaji na kuanzisha shughuli zinazowaingizia kipato.
‘WAKULIMA WATUMIE WATAALAMU’
Lukumay aliwataka wakulima kuhakikisha wanasajiliwa katika mifumo ya Serikali ili waweze kupata kwa urahisi ruzuku ya mbegu na mbolea, huku akisisitiza umuhimu wa huduma za ugani.
Alisema maofisa kilimo wanapaswa kuongeza elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya pembejeo, teknolojia na mbinu bora za uzalishaji.
“Wakulima waweze kusajiliwa kwenye mfumo ili iwe rahisi kupata ruzuku ya mbegu, vilevile na mbolea. Pia wapate maelekezo mbalimbali kwa ajili ya kuboresha kilimo ili wapate mazao yanayoridhisha yenye tija,” alisema.
MSUMI: MIKOPO ITUMIKE KUONGEZA UZALISHAJI
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Suleiman Msumi, alisema halmashauri inaendelea kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kila baada ya miezi mitatu.
Alisema mikopo hiyo inalenga kuongeza mitaji katika kilimo, mifugo na shughuli nyingine za ujasiriamali.
“Tunayo mikopo yetu ya asilimia 10 ambayo kila baada ya miezi mitatu tunatoa. Wanawake, vijana na ndugu zetu wenye ulemavu wanapaswa kuchangamkia mikopo hii isiyokuwa na riba ili waweze kuongeza mitaji yao katika kilimo na mifugo, kuzalisha zaidi na kukuza kipato,” alisema.
Msumi alisema halmashauri ina zaidi ya vikundi 200 vilivyosajiliwa katika kanzidata yake, huku baadhi vikiwa vimejikita katika kilimo, mifugo na ujasiriamali.
Alisema huduma za maafisa ugani na maafisa mifugo zimeanza kuleta mabadiliko kwa wakulima na wafugaji, hususan katika kilimo cha mbogamboga na ufugaji wa kisasa.
TUZO ZIWE CHACHU
Katika ziara hiyo, Lukumay alikabidhi vyeti na fedha kwa baadhi ya wakulima na wajasiriamali waliofanya vizuri katika kilimo, ufugaji na ubunifu.
Aliwataka washindi hao kutumia mafanikio yao kuwa mabalozi wa kilimo chenye tija na kuwahamasisha wananchi wengine kutumia fursa za Serikali.
Alisema tuzo hizo zisitafsiriwe kama mwisho wa safari, bali ziwe chachu ya kuongeza uzalishaji na kushirikisha wengine maarifa waliyoyapata.
Lukumay pia aliwataka wananchi kuendelea kulinda amani na utulivu nchini, akisema mazingira hayo ni msingi wa shughuli za kiuchumi na uzalishaji.
“Tuendelee kulinda amani katika nchi yetu. Bila amani leo tusingekuwa na watu wengi katika maonesho haya. Tunaipenda Serikali yetu ambayo nayo inatupenda,” alisema.
Ends .











إرسال تعليق