VERONICA KIDEMI AFUNGUKA MAZITO KWENYE KHANGA GALA, BAADA YA KUKATWA KIGANJA CHA MKONO NA MUMEWE,ALIPATWA NA AFYA YA AKILI

VERONICA KIDEMI AFUNGUKA MAZITO  KWENYE KHANGA GALA, BAADA YA KUKATWA KIGANJA CHA MKONO NA MUMEWE,ALIPATWA NA AFYA YA AKILI

Na Arusha Digital | Arusha

Veronica Kidemi ametoa ushuhuda mzito wa maisha yake, akieleza jinsi alivyofanikiwa kurejea katika afya njema ya akili baada ya kupitia tukio la kutisha la kukatwa kiganja cha mkono wake wa kulia na aliyekuwa mume wake.

Kidemi alitoa ushuhuda huo katika jukwaa la Khanga Gala lililofanyika jijini Arusha, ambapo alizungumza mbele ya mamia ya washiriki waliohudhuria hafla hiyo iliyolenga kuhamasisha wanawake kuhusu ujasiri, afya ya akili na kujikwamua kutoka katika changamoto mbalimbali za maisha.

Akisimulia safari yake, alisema maisha yake yalibadilika ghafla baada ya tukio hilo la ukatili ambalo mbali na kumuacha na ulemavu wa kudumu, pia lilimuathiri kisaikolojia na kumuingiza katika kipindi kigumu cha msongo wa mawazo.

“Nilipoteza sehemu ya mwili wangu, lakini kubwa zaidi nilipoteza amani ya moyo. Nilikuwa na maswali mengi, maumivu makubwa na wakati mwingine nilihisi kama maisha yamefika mwisho,” alisema Kidemi.

Alieleza kuwa baada ya tukio hilo alikumbwa na huzuni, hofu na mawazo yaliyomfanya kushindwa kuamini kama angeweza kuendelea na maisha ya kawaida, hasa kutokana na majukumu ya kulea watoto na kujitegemea.

Hata hivyo, alisema kupitia msaada wa wataalamu wa afya ya akili, familia, marafiki na imani yake kwa Mungu, alianza hatua kwa hatua kurejesha matumaini na kupona majeraha ya ndani yaliyokuwa yakimsumbua.

Kwa mujibu wa Kidemi, alijifunza kuwa uponyaji wa kweli hauhusiani tu na mwili bali pia na akili na moyo, akisisitiza kuwa mtu anaweza kuonekana amepona nje lakini bado akawa anateseka ndani endapo hatapata msaada wa kisaikolojia.

“Nilijifunza kujikubali. Nilijifunza kuishi na hali yangu mpya. Nilijifunza kuwa thamani yangu haijapungua kwa sababu nimepoteza mkono. Leo ninaishi kwa matumaini na ninaendelea kupambana kwa ajili ya watoto wangu na ndoto zangu,” alisema.

Alitumia nafasi hiyo kuwahimiza wanawake wanaokumbana na ukatili wa kijinsia kutafuta msaada mapema na kutokubali kunyanyasika kimya kimya kwa kuhofia aibu au maneno ya watu.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuzungumzia afya ya akili katika jamii, akieleza kuwa changamoto nyingi zinazowakumba watu huanza kwa majeraha ya kihisia ambayo yasipotibiwa yanaweza kuathiri maisha kwa kiwango kikubwa.

Washiriki wa Khanga Gala waliguswa na ushuhuda huo, huku wengi wakimpongeza kwa ujasiri wake wa kusimama hadharani na kueleza safari yake ya maumivu na ushindi, hatua iliyotafsiriwa kama chanzo cha matumaini kwa wanawake wengi wanaopitia changamoto mbalimbali nchini.

Ushuhuda wa Veronica Kidemi umeendelea kuibua mjadala kuhusu umuhimu wa kulinda afya ya akili, kupinga ukatili wa kijinsia na kuwapa nguvu manusura wa matukio ya kikatili ili waweze kurejea katika maisha ya kawaida na kutimiza ndoto zao.





Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم