ILO YASISITIZA ULINZI WA HAKI ZA WAFANYAKAZI WAHAMAJI

 ILO YASISITIZA ULINZI WA HAKI ZA WAFANYAKAZI WAHAMAJI

Na Arushadigital | Mombasa-KENYA

SHIRIKA la Kimataifa la Kazi Duniani (ILO) limezitaka vyombo vya habari katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuandika habari zinazolinda haki, hadhi na mchango wa wafanyakazi wahamaji, badala ya kuangazia zaidi changamoto na kasoro zinazowakabili.

Wito huo umetolewa na Mshauri Mkuu wa Kiufundi wa ILO, Aida Awel, wakati akifungua warsha ya kuwajengea uwezo viongozi wa vyama vya wafanyakazi wa wanahabari kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na Kati inayofanyika mjini Mombasa, Kenya.

Awel amesema wahamaji wana mchango mkubwa katika uchumi wa nchi wanakotoka na wanakoishi kupitia fedha wanazotuma kwa familia zao na uwekezaji wanaoufanya, lakini mchango huo bado haupewi uzito unaostahili katika vyombo vya habari.

“Wahamaji wamekuwa wakituma fedha zinazochangia ukuaji wa uchumi wa nchi zao na za nchi wanazoishi, lakini bado hawaandikwi vizuri katika vyombo vya habari,” alisema Awel.

Alibainisha kuwa kwa sasa duniani kuna zaidi ya wahamiaji milioni 250, huku Afrika ikiwa na zaidi ya wahamiaji milioni 21 na takribani Waafrika milioni 19.5 wanaoishi nje ya bara hilo.

Kwa mujibu wa Awel, Afrika hupokea zaidi ya dola za Marekani bilioni 100 kwa mwaka kutoka kwa wahamaji, sawa na zaidi ya Shilingi trilioni 262 za Tanzania, lakini mchango huo hauonekani vya kutosha katika simulizi zinazoripotiwa na vyombo vya habari.

“Tunashuhudia Waafrika wengi wakicheza soka katika mataifa ya Ulaya na sehemu nyingine duniani. Wengi wao wanachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi zao kupitia fedha wanazotuma nyumbani. Uhamaji wa kutafuta kazi kwa kufuata sheria si kosa wala dhambi,” alisisitiza.

Akizungumza katika warsha hiyo, Rais wa Shirikisho la Wanahabari Afrika (FAJ), Omar Faruk Osman, aliwataka wanahabari kuzingatia usahihi na uwiano katika kuripoti masuala ya uhamaji ili kuepuka upotoshaji wa umma.

Osman alisema uhamaji wa wafanyakazi ni moja ya njia zinazoweza kusaidia kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana barani Afrika, huku akizitaka serikali kuweka mazingira bora yatakayowezesha vijana kupata ajira halali ndani na nje ya nchi zao.

“Serikali nyingi za Afrika zimekuwa zikiahidi kupambana na tatizo la ajira kwa vijana, lakini bado hazijaweka mazingira rafiki ya kuwawezesha vijana kupata fursa za kazi katika nchi nyingine kwa njia salama na halali,” alisema.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Wanahabari Afrika Mashariki (FEAJ), Eric Oduor, alisema warsha hiyo inalenga kuwajengea uwezo viongozi wa vyama vya wanahabari ili wakarejee katika nchi zao na kutoa mafunzo kwa wanahabari kuhusu namna bora ya kuripoti masuala ya uhamaji.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), Mussa Juma Siwayombe, aliwataka viongozi wa Afrika kuweka sera na sheria rafiki zitakazowezesha vijana, wakiwemo wanahabari, kupata mikataba bora ya ajira ndani na nje ya nchi zao.

Warsha hiyo imeandaliwa na ILO kwa kushirikiana na Shirikisho la Wanahabari Afrika (FAJ), Shirikisho la Wanahabari Afrika Mashariki (FEAJ) na Chama cha Waandishi wa Habari Kenya (KUJ).

Tanzania imewakilishwa na viongozi wa JOWUTA, akiwemo Mwenyekiti wa Taifa, Mussa Juma Siwayombe, pamoja na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini, Caren-Tausi Mbowe.

Washiriki wa warsha hiyo wametoka katika nchi za Comoro, Djibouti, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda.



Post a Comment

أحدث أقدم