KESI YA KUMNG'OA UBUNGE BABA LEVO KIGOMA MJINI YACHUKUA SURA MPYA

KESI YA KUMNG'OA UBUNGE BABA LEVO KIGOMA MJINI YACHUKUA SURA MPYA

Na Arushadigital | KIGOMA 

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Kigoma, imekubali ombi la walalamikaji katika kesi ya uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Mjini la kuongezewa muda wa kuwasilisha maelezo ya mashahidi wao katika shauri linalompinga Mbunge wa jimbo hilo, Clayton Revocatus Chipando maarufu kama Baba Levo.

Uamuzi huo ulitolewa Juni 18, 2026 na Jaji Victoria Nongwa baada ya kuridhika kuwa walalamikaji walikuwa na sababu za msingi za kuomba nyongeza ya muda kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya ushahidi wao.

Kwa mujibu wa walalamikaji, baada ya usikilizwaji wa awali wa shauri hilo kukamilika Juni 15, 2026 saa 12 jioni, walibakiwa na muda mfupi wa kuandaa maelezo ya mashahidi muhimu. Walieleza kuwa baadhi ya mashahidi walikuwa nje ya Mkoa wa Kigoma wakati wa maandalizi ya nyaraka za Mahakama, jambo lililosababisha ugumu wa kukamilisha taratibu ndani ya muda uliopangwa.

Wakiiomba Mahakama, walalamikaji walidai kuwa nyongeza ya muda ilikuwa muhimu ili kuhakikisha ushahidi wote unaokusudiwa kutumika katika shauri hilo unawasilishwa kwa kuzingatia matakwa ya sheria na kanuni za uchaguzi.

Akitoa uamuzi wake, Jaji Nongwa alisema Mahakama imeridhika kuwa maombi hayo yana msingi wa kisheria na kwamba walalamikaji walifuata taratibu zote zinazotakiwa, hivyo kuidhinisha ombi la kuongezewa muda wa kuwasilisha maelezo ya maandishi ya mashahidi wao.

Baada ya uamuzi huo, Wakili Thomas Msasa anayemwakilisha mlalamikiwa wa pili, Clayton Chipando, alisema upande wake umeupokea uamuzi huo na utaendelea kushiriki kikamilifu katika mwenendo wa shauri kwa mujibu wa sheria.

Katika kesi hiyo, walalamikaji wanapinga ushindi wa Baba Levo kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, wakidai kuwa uchaguzi huo ulikuwa na ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi pamoja na madai ya vitendo vya rushwa na udini.

Mahakama imepanga kuendelea na usikilizwaji wa shauri hilo Julai 6, 2026, huku walalamikaji wakipewa muda wa saa 48 kuwasilisha maelezo ya ushahidi wa mashahidi watakaotegemea katika kesi hiyo.

Ends**

Post a Comment

أحدث أقدم