EAC YAPENDEKEZA BAJETI YA DOLA MILIONI 110.8 KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIKANDA


EAC YAPENDEKEZA BAJETI YA DOLA MILIONI 110.8 KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIKANDA

Na Joseph Ngilisho, AEUSHA

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) imependekeza bajeti ya Dola za Marekani milioni 110.8 kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kukuza biashara, kuboresha miundombinu, kuimarisha usalama na kuharakisha mageuzi ya kidijitali kwa manufaa ya wananchi wa nchi wanachama.

Akizungumza mbele ya Kamati ya Masuala ya Jumla ya Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Stephen Patrick Mbundi, alisema bajeti hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia mkakati wa kuimarisha ustahimilivu wa uchumi wa kikanda kupitia usalama, uhamasishaji wa mapato ya ndani na matumizi ya teknolojia katika kuharakisha maendeleo endelevu.

Alieleza kuwa kati ya fedha hizo, Dola milioni 64.7 sawa na asilimia 58 ya bajeti yote zinatarajiwa kuchangiwa na nchi wanachama, huku Dola milioni 46.1 sawa na asilimia 42 zikitarajiwa kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Kwa mujibu wa Balozi Mbundi, mpango huo unaendana na dira ya EAC ya kujenga jumuiya yenye ushindani wa kiuchumi, ustawi na maendeleo jumuishi kwa wananchi zaidi ya milioni 300 wanaoishi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Akiwasilisha tathmini ya utekelezaji wa shughuli za mwaka uliopita, alisema biashara ya ndani ya EAC imeongezeka kwa asilimia 28 mwaka 2025 na kufikia Dola za Marekani bilioni 19.3, hatua iliyochangiwa na kuondolewa kwa vikwazo visivyo vya ushuru pamoja na kuanzishwa kwa mfumo wa kidijitali wa dhamana ya forodha unaorahisisha usafirishaji wa bidhaa katika nchi wanachama.

Katika sekta ya afya, Katibu Mkuu huyo alisema Jumuiya imeendelea kuimarisha huduma za afya kwa kuendesha vituo maalumu vya ubora ambapo wagonjwa zaidi ya 12,500 wamehudumiwa. Aidha, maabara 10 zinazotembea zimepelekwa katika maeneo mbalimbali ya ukanda huo ili kuongeza utayari wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa hatari, ikiwemo ugonjwa wa Ebola.

Katika kuendeleza ubunifu na matumizi ya teknolojia, Balozi Mbundi alisema vijana 16 kutoka nchi wanachama walipatiwa mafunzo maalumu pamoja na ruzuku ya Dola 10,000 kila mmoja kwa ajili ya kuendeleza miradi ya ubunifu wa kidijitali inayolenga kutoa suluhisho kwa changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi katika ukanda huo.

Alisisitiza kuwa bajeti ya mwaka 2026/2027 inalenga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika miaka iliyopita na kuimarisha nafasi ya EAC kama kitovu cha biashara, uwekezaji, ubunifu na maendeleo ya kijamii barani Afrika.

Wajumbe wa Kamati ya Masuala ya Jumla ya EALA wanatarajiwa kujadili mapendekezo hayo kabla ya kuwasilishwa rasmi katika vikao vya Bunge la Afrika Mashariki kwa hatua zaidi za kisheria na bajeti.






Post a Comment

أحدث أقدم