ATC YAFUNGUA WIKI YA UTAFITI, UBUNIFU NA UJASIRIAMALI;HYPORMED HEALTHCARE YATOA MILIONI 20 KUSAIDIA MIRADI YA WANAFUNZI

 ATC YAFUNGUA WIKI YA UTAFITI, UBUNIFU NA UJASIRIAMALI;HYPORMED HEALTHCARE YATOA MILIONI 20 KUSAIDIA MIRADI YA WANAFUNZI

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

CHUO cha Ufundi Arusha (ATC) kimefungua rasmi Wiki ya Utafiti, Ubunifu na Ujasiriamali kwa mwaka 2026, huku Mkuu wa chuo hicho, Profesa Mussa Chacha, akiwahimiza vijana kutumia maarifa, tafiti na teknolojia kutatua changamoto zinazoikabili jamii na kuchochea maendeleo ya taifa.

Akizungumza june 15,2026 wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo yanayofanyika chuoni hapo kwa mara ya tatu tangu kuanzishwa kwake, Profesa Chacha alisema maendeleo ya Tanzania yanategemea kwa kiwango kikubwa uwezo wa vijana kubuni suluhisho bunifu katika sekta mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kiteknolojia.

Alisema wiki hiyo ni jukwaa muhimu linalowawezesha wanafunzi, walimu na watafiti kuonesha matokeo ya tafiti zao, bunifu mbalimbali pamoja na miradi ya ujasiriamali inayolenga kutoa majawabu ya changamoto zinazoikabili jamii.

“Lengo la maonesho haya si kuonesha tu kile kinachofanyika darasani, bali kuonesha namna elimu ya ufundi na teknolojia inavyoweza kubadilishwa kuwa suluhisho la matatizo halisi yanayoikabili jamii yetu,” alisema Profesa Chacha.

Alieleza kuwa ATC imeendelea kuimarisha utamaduni wa kufanya tafiti na kuhamasisha ubunifu miongoni mwa wanafunzi, hatua ambayo imewezesha kuzalishwa kwa teknolojia mbalimbali zinazoweza kutumika katika sekta za nishati, maji, ujenzi, kilimo, usafirishaji na mifumo ya kidijitali.


Kwa mujibu wa Profesa Chacha, baadhi ya bunifu zilizowahi kuoneshwa katika maonesho hayo zimeendelea kuboreshwa na kufikia hatua ya kutumika katika taasisi mbalimbali nchini, jambo linalodhihirisha uwezo mkubwa wa vijana wa Kitanzania katika kuzalisha teknolojia zinazoweza kuchochea maendeleo ya taifa.

Alisisitiza kuwa dunia ya sasa inabadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, hivyo taasisi za elimu zina wajibu wa kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa yanayowawezesha kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira na mazingira ya biashara yanayobadilika kila siku.

“Tunataka kuona wanafunzi wetu wanahitimu wakiwa si watafuta ajira pekee, bali wawe wabunifu, wajasiriamali na waajiri watakaotengeneza fursa kwa wengine kupitia maarifa na ujuzi walioupata chuoni,” alisema.

Katika maonesho ya mwaka huu, washiriki wamewasilisha miradi mbalimbali inayohusisha teknolojia za nishati jadidifu, matumizi ya akili mnemba (Artificial Intelligence), mifumo ya kidijitali, vifaa vya uhandisi pamoja na miradi ya ujasiriamali inayolenga kuongeza ajira kwa vijana.

Wakati huo huo, sekta binafsi imeonesha kuunga mkono juhudi za kukuza ubunifu nchini baada ya Kampuni ya Hypmed Healthcare Limited kutangaza msaada wa Shilingi milioni 20 kwa ajili ya kusaidia miradi bora ya wanafunzi wanaoshiriki maonesho hayo.


Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Bw. Deogratias Kiduduye, alisema vijana wana nafasi kubwa ya kuleta mageuzi ya maendeleo kupitia mawazo yao ya kibunifu, hivyo wanapaswa kupewa mazingira na rasilimali zitakazowawezesha kuyageuza mawazo hayo kuwa miradi halisi yenye manufaa kwa jamii.

“Ubunifu ni injini muhimu ya maendeleo ya taifa. Kupitia teknolojia na tafiti zinazofanywa na vijana wetu tunaweza kupata majawabu ya changamoto nyingi zinazotukabili katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na biashara,” alisema Kiduduye.

Alisema yeye pamoja na kampuni yake walialikwa kushiriki katika maonesho hayo kama wadau wa maendeleo na wahitimu wa ATC, kwa lengo la kuwahamasisha wanafunzi kutumia elimu na teknolojia kama nyenzo za kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Kiduduye alibainisha kuwa Hypmed Healthcare Limited ni kampuni inayojihusisha na usambazaji wa vifaa tiba nchini pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya ili kuhakikisha matumizi sahihi ya teknolojia za kisasa katika utoaji wa huduma za afya.

Alisema baada ya kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho, amevutiwa na kiwango cha ubunifu kilichooneshwa na wanafunzi wa ATC, akieleza kuwa baadhi ya miradi ina uwezo mkubwa wa kutatua changamoto za kijamii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi endapo itapatiwa usaidizi unaostahili.

“Kuna ubunifu mkubwa unaofanywa na vijana hawa. Kazi yetu kama wadau ni kuwapa moyo, kuwashauri na kuwasaidia ili mawazo yao yaweze kufikia hatua ya utekelezaji na kuwanufaisha wananchi,” alisema.

Katika hatua ya kuunga mkono jitihada hizo, kampuni hiyo imetangaza kutoa Shilingi milioni 20 kwa vikundi vinne vya wabunifu vitakavyoibuka kuwa bora zaidi katika maonesho hayo, ambapo kila kikundi kitapokea Shilingi milioni tano kwa ajili ya kuendeleza miradi yao.

Alisema fedha hizo zitatolewa baada ya tathmini ya kina kufanywa na uongozi wa chuo kwa kushirikiana na wataalamu mbalimbali ili kuhakikisha msaada huo unawanufaisha wabunifu wenye miradi yenye tija na uwezo wa kutatua changamoto za jamii.

Kiduduye alisema uwekezaji huo ni sehemu ya dhamira ya kampuni yake katika kuwekeza kwenye vipaji, maarifa na ubunifu wa vijana ambao ni msingi wa maendeleo endelevu ya taifa.

“Tunataka kuona mawazo ya vijana yanageuzwa kuwa miradi halisi inayozalisha ajira, kuongeza tija na kuboresha maisha ya Watanzania. Huu ni mwanzo wa ushirikiano mkubwa kati ya sekta binafsi na taasisi za elimu katika kukuza ubunifu nchini,” alisema.

Naye Profesa Chacha alieleza kuwa ushiriki wa wadau wa sekta binafsi katika maonesho hayo ni hatua muhimu inayosaidia kuunganisha elimu, utafiti na mahitaji halisi ya soko, huku akisisitiza kuwa chuo kitaendelea kuwekeza katika miundombinu ya utafiti na ubunifu ikiwemo karakana na vituo vya kisasa vya teknolojia.

Wiki ya Utafiti, Ubunifu na Ujasiriamali ya ATC imeendelea kuwa moja ya matukio muhimu ya kitaaluma katika Mkoa wa Arusha, ikilenga kukuza utamaduni wa utafiti, ubunifu na ujasiriamali miongoni mwa vijana, huku ikijenga daraja kati ya taasisi za elimu, sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika kuibua teknolojia na suluhisho za changamoto za jamii.







Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم