ONGEZEKO LA BILIONI 61 OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI LAIBUA MATUMAINI MAPYA ,MWANASHERIA MKUU AJIVUNIA WELEDI UTENDAJI KAZI AHIMIZA NIDHAMU

MWANASHERIA MKUU : ONGEZEKO LA BAJETI  YA BILIONI 61 KATIKA OFISI YAKE NI MATOKEO YA UFANISI KATIKA UTENDAJI KAZI

 Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Hamza Johari amesema ongezeko la bajeti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufikia shilingi bilioni 61.913 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ni matokeo ya utendaji bora wa taasisi hiyo pamoja na kuongezeka kwa imani ya Serikali katika majukumu yake ya kisheria.

Johari ameyasema hayo leo April 27,2026 katika Mkutano wa Pili wa Baraza la Wafanyakazi wa ofisi ya mwanasheria Mkuu wa serikali , uliofanyika jijini Arusha, ambapo alisema ongezeko hilo la takriban asilimia 49 litaongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kulinda maslahi ya Taifa na kuwataka watumishi kuzidisha uadilifu na nidhamu katika utumishi wao.

Alieleza kuwa kati ya bajeti hiyo, shilingi bilioni 4.8 zimetengwa kwa mishahara, bilioni 52.2 kwa matumizi mengineyo na bilioni 4 kwa miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi na upanuzi wa ofisi katika mikoa mbalimbali.

“Tunaendelea kuimarisha mifumo ya sheria kwa sababu ndiyo dira ya maendeleo ya nchi. Bila sheria imara, Taifa linaweza kupoteza mwelekeo,” alisema Johari.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, Samweli Maneno, alieleza kuwa ofisi hiyo imeendelea kupata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu yake, hususan katika usimamizi wa mikataba ya Serikali na matumizi bora ya rasilimali.

Alisema mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri uliopo kati ya watumishi na menejimenti, hali iliyochangia kuimarika kwa utendaji na kuongezeka kwa tija katika kazi.

Maneno alibainisha kuwa pamoja na changamoto zilizopo, ofisi imeendelea kusonga mbele kwa kuwekeza katika rasilimali watu, kuboresha mazingira ya kazi na kutoa fursa za mafunzo zinazowawezesha watumishi kuendana na mabadiliko ya kitaaluma.

Alisisitiza kuwa dhamira ya baraza ni kuhakikisha maslahi ya watumishi yanazingatiwa sambamba na kuongeza ufanisi wa taasisi, akiwataka watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na mshikamano.

Katika hatua nyingine, mkutano huo ulienda sambamba na uchaguzi wa viongozi wa Baraza la Wafanyakazi, ambapo viongozi wapya walichaguliwa kuongoza baraza hilo, hatua inayotajwa kuwa ni muhimu katika kuimarisha uwazi na ushirikishwaji wa watumishi katika maamuzi ya taasisi.

Akitoa maoni ya wafanyakazi, Katibu wa Baraza hilo, William Mudogo, alisema licha ya maboresho ya mazingira ya kazi, suala la mishahara bado ni changamoto kubwa inayohitaji kupewa kipaumbele.

“Mishahara ni msingi wa kuongeza morali na ufanisi kazini. Tunaomba Serikali iangalie kwa upya suala hili,” alisema Mudogo.

Alipongeza pia maboresho ya huduma za afya, vitendea kazi, mafunzo na ujenzi wa ofisi mpya mikoani, akisema yameongeza tija na ari ya watumishi.

Baraza hilo lilipongeza Serikali kwa kuanzisha na kuimarisha ofisi za Mwanasheria Mkuu katika mikoa ya Kagera, Mtwara, Tanga na Mbeya, huku likiomba kasi ya upanuzi iongezwe ili huduma za kisheria ziwafikie wananchi wengi zaidi.

Katika msisitizo wake mwanasheria Mkuu wa serikali alitoa rai kwa wafanyakazi kuhakikisha suala la nidhamu kazini linapewa kipaumbele, ambapo alisema mafanikio ya taasisi yoyote ya umma yanategemea uwajibikaji na nidhamu ya kila mtumishi.

“Nidhamu ndiyo msingi wa mafanikio kazini. Bila nidhamu, hata uwezo mkubwa hauleti matokeo yanayotarajiwa,” alisema.




Ends..

Post a Comment

0 Comments