TAHADHARI YA USALAMA YATIKISA HAFLA YA WAANDISHI IKULU YA MAREKANI
By Arushadigital
Mtu aliyekamatwa kufuatia tukio la ufyatuaji risasi lililotokea usiku wa kuamkia Jumamosi katika hoteli iliyokuwa ikiandaa hafla ya Chakula cha Waandishi wa White House ametambuliwa rasmi, kwa mujibu wa taarifa kutoka mtandao wa Marekani CBS News, mshirika wa BBC, baada ya kunukuu vyanzo vya vyombo vya usalama.
Mshukiwa huyo ametajwa kuwa Cole Tomas Allen (31), mkazi wa Torrance, eneo lililoko kusini magharibi mwa Los Angeles katika jimbo la California.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Allen alikamatwa ndani ya Washington Hilton, ambako hafla hiyo ilikuwa ikiendelea, baada ya kuzuiliwa haraka na maafisa wa usalama waliokuwa doria. Inadaiwa kuwa mara baada ya kukamatwa, mshukiwa huyo aliwaeleza maafisa kuwa nia yake ilikuwa kuwalenga kwa risasi baadhi ya maafisa wa utawala wa Rais wa zamani Donald Trump.
Vyanzo viwili vya usalama vilivyozungumza na CBS vimeeleza kuwa kati ya risasi tano hadi nane zilifyatuliwa wakati wa tukio hilo, jambo lililozua taharuki kubwa miongoni mwa wageni na washiriki wa hafla hiyo ya kitaifa.
Hata hivyo, hadi sasa mamlaka hazijatoa taarifa kamili kuhusu iwapo kuna majeruhi au athari nyingine zilizotokana na tukio hilo, huku uchunguzi ukiendelea kubaini undani wa shambulio hilo na motisha ya mshukiwa.
Ends.




0 Comments