MWANASHERIA MKUU ATAKA NIDHAMU, BIDII KUONGEZA UFANISI KATIKA UTENDAJI KAZI ILI KUFIKIA MALENGO OFISI YAKE

 MWANASHERIA MKUU ATAKA NIDHAMU, BIDII KUONGEZA UFANISI KATIKA UTENDAJI KAZI SERIKALINI 

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, amewataka watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na weledi ili kuhakikisha taasisi hiyo inatimiza kikamilifu wajibu wake wa kikatiba na kisheria kwa manufaa ya Taifa.

Akizungumza katika Mkutano wa Pili wa Baraza la Wafanyakazi wa ofisi hiyo uliofanyika jijini Arusha Aprili 27, 2026, Johari alisisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya muda wa kazi pamoja na uwajibikaji wa kila mtumishi katika nafasi yake.

Alieleza kuwa ufanisi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali unategemea kwa kiasi kikubwa nidhamu, uadilifu na mshikamano wa watumishi wake, huku akisisitiza kuwa utoaji wa huduma bora za kisheria unapaswa kuendana na matarajio ya wadau wa Serikali na wananchi kwa ujumla.

“Tuna wajibu wa kuhakikisha tunatoa huduma za kisheria kwa ubora, ufanisi na tija inayotarajiwa. Hili linawezekana endapo kila mmoja atatekeleza majukumu yake kwa nidhamu na kujituma,” alisema Johari.

Aidha, alibainisha kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya kisheria ili kuhakikisha inakuwa imara na yenye kuongoza mwelekeo wa maendeleo ya Taifa.

“Sheria ni msingi wa maendeleo ya nchi. Bila mifumo imara ya kisheria, Taifa linaweza kupoteza dira yake,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, Samweli Maneno, alisema ofisi hiyo imeendelea kupata mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yake kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya watumishi na menejimenti.

Alieleza kuwa hali hiyo imechangia kuimarika kwa utendaji kazi, hususan katika usimamizi wa mikataba ya Serikali na matumizi bora ya rasilimali za umma.

Maneno aliongeza kuwa pamoja na changamoto zilizopo, ofisi imeendelea kuboresha mazingira ya kazi, kuwekeza katika rasilimali watu na kutoa mafunzo yanayowawezesha watumishi kuendana na mabadiliko ya kitaaluma.

Alisisitiza kuwa Baraza la Wafanyakazi litaendelea kusimamia maslahi ya watumishi huku likihimiza uwajibikaji na kuongeza ufanisi wa taasisi hiyo.

Katika hatua nyingine, mkutano huo ulienda sambamba na uchaguzi wa viongozi wa Baraza la Wafanyakazi, hatua inayolenga kuimarisha uwazi na ushirikishwaji wa watumishi katika maamuzi ya taasisi.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi, Katibu wa Baraza hilo, William Mudogo, alisema pamoja na maboresho yanayoendelea kufanyika, bado kuna haja ya kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi ili kuongeza morali na ufanisi kazini.

Alipongeza juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya, upatikanaji wa vitendea kazi, mafunzo pamoja na ujenzi wa ofisi mpya katika mikoa mbalimbali, akisema hatua hizo zimeongeza ari ya kazi kwa watumishi.

Baraza hilo pia lilipongeza hatua ya kuanzishwa na kuimarishwa kwa ofisi za Mwanasheria Mkuu katika baadhi ya mikoa, likieleza kuwa upanuzi huo unasaidia kusogeza huduma za kisheria karibu zaidi na wananchi.

Akihitimisha, Johari alisisitiza kuwa mafanikio ya taasisi yoyote ya umma yanategemea nidhamu na uwajibikaji wa watumishi wake, akiwataka kuendelea kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

“Nidhamu ndiyo msingi wa mafanikio. Bila nidhamu, hata uwezo mkubwa hauwezi kuleta matokeo chanya,” alisema.






Post a Comment

0 Comments